KOCHA Mkuu wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema kuwa hawakuwa na namna ya kuweza kushinda mchezo wao wa Kombe la FA mbele ya Leicester City kwa kuwa wachezaji wake walikuwa wamechoka.
Solksajer amesema kuwa wachezaji hawakuwa na maajabu kwenye mchezo huo kwa kuwa ni muda mfupi wametoka kucheza na wamesafiri muda mrefu jambo ambalo limewafanya washindwe kuonyesha makeke yao uwanjani.
United imetolewa kwenye Kombe la FA hatua ya robo fainali kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Leicester City ikiwa ni siku tatu baada ya kutoka kushinda kwenye mchezo wa Europa League mbele ya AC Milan pale San Siro na United ilishinda bao 1-0 ambalo lilifungwa na Paul Pogba.
Mabao ya Leicester City yalifungwa na Kelechi Iheanacho dakika ya 24 na 78 na Youri Tielemans dakika ya 52 huku lile la Manchester United likifungwa na Mason Greenwood dakika ya 38.
Kocha huyo amesema kuwa hali inaeleweka kwa wachezaji namna walivyo pamoja na kushindwa kushinda Uwanja wa King Power kwa kuwa wanacheza mechi moja kila baada ya siku tatu jambo lisilo la kawaida.
"Hatukuwa na chaguo na inaeleweka kwamba kila baada ya siku tatu wachezaji wanacheza na hilo ni jambo kubwa na kila mechi ina ushindani. Tumekuwa tukitumia muda pia kwenye safari kwa kuwa tunahitaji kufanikiwa ni lazima hili tulimudu kwenye maisha yetu ya soka.
"Ni lazima tujifunze na tuwe na hali ya kujiamini kwa ajili ya mechi zetu zijazo, kazi bado ni ngumu na mechi zinatukabili kila wakati," .
0 Comments