TANGAZA NASI

header ads

Madereva boda boda wala Ugoro washtukiwa,Polisi watoa onyo

 



Na Amiri Kilagalila,Njombe


Jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani nchini wamesema wamebaini uwepo wa madereva wa boda boda wanaohatarisha usalama kutokana na ulevi wa kupindukia hususani matumizi ya ugoro na kuwataka kuacha mara moja kabla sheria dhidi yao hazijachukuliwa


Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani (T) Afande SACP Wilbrod. Mutafungwa amebainisha hayo mkoani Njombe wakati akizungumza na kundi  moja wapo la watumiaji wa barabara ambao ni  madereva wa pikipiki (Bodaboda).


“Wapo boda boda wengine wanakula Ugoro yaani unaongea nae unaona hana harufu ya pombe kumbe ameshakula Ugoro karibia pakiti nzima na huu Ugoro ni hatari utakuta mtu anaendesha piki piki anakupita mpaka anataka kupaa”alisema Mutafungwa


Aidha amewakumbusha bodaboda hao kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali ambazo wamekuwa wakisababisha nakupelekea vifo, majeruhi na uharibifu wa vyombo na mali kwa kuendesha kwa mwendokasi.


“Sisi tunatamani wewe ukiwa salama zaidi ili kesho uendelee na shughuli za uzalishaji mali,ukipata shida barabarani familia yako ndio inayo athirika lakini mwisho wa siku taifa linakosa mtu aliyekuwa na mchango mkubwa katika serikali,hatutaki mteketee kwa kukosa maarifa ndio maana kila wakati tunawapa elimu”aliongeza Mutafungwa


Vile vile amewataka kuhudhuria mafunzo ya udereva kabla ya kuanza kuendesha bodaboda barabarani ili kupata uelewa wa sheria, alama na michoro hivyo kuepuka ajali ambazo wangeweza kupata.


Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Njombe Jane Warioba,amepiga marufuku kwa madereva hao kumkabidhi boda boda mtu yeyote asiyepata mafunzo wala kuwa na leseni ya udereva.


“Mnawapatia watu piki piki ambao wanajiita wakata kiu,hawajahudhuria mafunzo wala hana leseni.Kwa hiyo acha kutoa piki piki kwa mtu ambaye hana mafunzo ya bara barani”alisema Jane Warioba


Mwenyekiti wa madereva boda boda halmashauri ya mji wa Makambako kwa niaba ya madereva hao ameshukuru kuendelea kukumbushwa huku akiliomba jeshi la polisi kuto choka kutoa elimu dhidi ya sheria za barabarani pamoja na udereva bora.

Post a Comment

0 Comments