Watu watatu wamekufa na wengine 24 wamejeruhiwa baada ya tetemeko la ardhi kupiga leo katika kisiwa cha Sulawesi, Indonesia. Shirika la kukabiliana na majanga la Indonesia limesema kuwa tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa 6.2 katika kipimo cha Richta.
Kwa mujibu wa Shirika la Jiolojia la Marekani, USGS, kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa kilomita sita kaskazini mashariki mwa mji wa Mamuju, na lilikuwa na kina cha kilomita 10.
Msemaji wa Shirika la kukabiliana na majanga la Indonesia, Raditya Jati amesema kuwa hoteli moja na ofisi ya gavana zimeharibiwa vibaya na tetemeko hilo la ardhi kwenye wilaya ya Majene.
Watu wapatao 2,000 wameondolewa kwenye nyumba zao na kupelekwa kwenye makaazi ya muda. Takriban nyumba 62, kituo cha afya na ofisi ya jeshi zimeharibiwa kwenye mji wa Mamuju ambao una takriban wakaazi 110,000.
0 Comments