Na Amiri Kilagalila,Njombe.
Mbunge wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe wakili Joseph Kamonga ameshiriki na wananchi katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa kwenye shule ya msingi Mbongo kata ya Manda sambamba na kuchangia mifuko 100 ya saruji ya shule hiyo na shule ya sekondari Manda ili kuendelea kupunguza changamoto kwenyeSawakwaajili sekta ya elimu.
Pamoja na kuchangia mifuko hiyo ya saruji mbunge huyo ametoa fedha taslimu laki tisa kwaajili ya ununuzi wa bati za kumalizia uezekaji wa ofisi ya kijiji cha Mbongo huku akiahidi kuchangia milioni moja kwaajili ya madawati katika shule ya sekondari Mchuchuma.
Vyumba hivyo viwili vya madarasa vinajengwa kwa nguvu ya wanaludewa wanaoishi ndani na nje ya wilaya ambao wameunda kundi la Whatsapp linalojadili Maendeleo ya wilaya na kuchangishana fedha kwa ajili ya kuboresha Maendeleo mbalimbali ya Wilayani yao pamoja na kundi la Mbongo family.
Mbunge huyo akiwa ni mmoja wa kundi hilo la Whatsapp la wilaya ya Ludewa amesema licha ya kutoa mchango ndani ya kundi lakini ameona aongeze mchango wake wa mifuko hiyo ya saruji ili kuhakikisha ujenzi huo unaenda bila kukwama.
Aidha ameyashukuru makundi hayo kwa kuonyesha ushirikiano wao katika kuleta maendeleo katika wilaya hiyo na kuwasihi kuendelea kujitoa katika kuleta maendeleo zaidi hata katika maeneo mengine ya wilaya hiyo yenye changamoto.
"Napenda niwashukuru Sana kundi la wilaya ya Ludewa pamoja na kundi la Mbongo family ambayo yametoa mchango mkubwa sana katika ujenzi huu wa madarasa haya, nami ni mmoja wa kundi la wilaya hivyo ninaimani kundi langu hili litaendeleza kuchangia Maendeleo ya wilaya yetu hata katika maeneo mengine pia", alisema Kamonga.
Naye mmoja wa kundi la Mbongo family alifika kuangalia maendeleo ya ujenzi huo kutokea jijini Dar es Salaam akiwakilisha kundi lake Obed Kasambara amesema wanatarajia ujenzi huo kukamilika haraka ili madarasa hayo yaanze kutumiwa hivyo amewaomba wanakikundi wenzie kuendeleza michango ili waweze kufikia malengo.
Pia amemuomba mhandisi wa majengo na timu yake kutoka wilayani kufika kwa wakati wanapohitajika ili ujenzi huo uende haraka.
" Mimi nimefika hapa nimekuta msingi umesha jengwa na ujenzi unaendelea kwa hatua nyingine, lakini jana mhandisi alipokuja akasema msingi upo chini Sana hivyo unatakiwa kupandishwa zaidi kwahiyo endapo wangekuja kukagua mapema sasa hivi tungekuwa tunaendelea na hatua nyingine badala ya kupandisha msingi", alisema Kasambara.
Naye mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mbongo Joseph Mapunda amewashukuru wadau wote wanaojitoa katika ujenzi huo na kuongeza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa saruji hivyo anaomba wadau hao kuendeleza michango yao ili waweze kupata saruji.
Amesema kwa upande wa wanakijiji wanajitoa katika kuchangia nguvu kazi ambapo wamekuwa wakichota maji, kusogeza mawe, mchanga na shughuli nyinginezo.
Aidha kwa upande wa mmoja wa wanachi wa kijiji hicho Chedi Mapunda amewashukuru makundi yote yanayotoa michango ya ujenzi huo na kusema kuwa madarasa hayo yatakuwa msaada mkubwa sana kwa watoto wao kwani madarasa wanayotumia Sasa ni machakavu.
0 Comments