TANGAZA NASI

header ads

Serikali kushusha rungu kwa wakopeshaji umiza wa pembejeo kwa wakulima

 


Na Amiri Kilagalila,Njombe


Halmashauri ya mji wa Njombe imejipanga kupambana na mashirika ya kilimo yanayotoa mikopo kandamizi ya pembejeo kwa wakulima kwa mgongo wa kutoa misaada yakiwa kwa kivuli cha NGO's wakati ni makampuni ya kibiashara yanayotafuta faida.


Serikali imejipanga kuendelea kufuatilia mashirika hayo kutokana na malalamiko kutoka kwa wakulima kuingia kwenye migogoro na mashirika hayo baada ya kushindwa kurejesha mikopo kutokana na ulaghai unaofanywa na baadhi ya mashirika pamoja na wakulima wengine kushindwa kufikia malengo ya uzalishaji wakati wa mavuno.


Onesmo Kamonga ni afisa ugani wa kata ya Iwungilo na Suzana Kiwele ni afisa kilimo wa kata ya Kifanya kwa niaba ya wakulima,wakizungumza katika kikao cha mrejesho wa mradi wa kilimo kutoka shirika la Highlands hope Umbrella (HHU) unaotekelezwa katika tarafa ya Igominyi Njombe mjini,wamesema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa wakulima wakilubuniwa pembejeo kwa kukopeshwa kwa bei naafuu ili hali wakati wa mavuno wamekuwa wakilipa zaidi ya makubaliano.




“Mkulima anapenda sana afanikiwe kwa hiyo wakiona shirika linatoa labda mbolea hawezi kuacha sasa tunapata malalamiko kwa kuwa awali mashirika yanakuja kwa lugha tamu ila mwisho wa siku baada ya mavuno liba yake inakuwa ni kubwa tofauti na walichokipata”alisema Suzana Kiwele


“Ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara mimi niwaombe wakulima wajenge msingi wa kujitegemea kuliko kuendesha kilimo kwa mikopo kwa kila kitu na wakopeshaji wengine wako kibiashara zaidi”alisema Onesmo Kamonga



Bethseba  Liduke ni mkurugenzi wa shirika la Highlands hope Umbrella (HHU) amesema kwa sasa wameingia katika kilimo ili kuongeza nguvu ya mabadiriko ya kilimo bora ufanisi na chenye tija mkoani Njombe,huku akiwashauri wakulima kuwa makini na mashirika yanayofika kwenye maeneo yao,pamoja na serikali kuendelea kupambana na mashirika umiza.


“Niwashauri wakulima wawe makini na haya mashirika yanayoingia kwenye maeneo yao,na tuombe sana serikali iweze kuingilia kati na kuwasaidia wakulima wanapongia kwenye migogoro na mashirika”alisema Beth Liduke


Bi,Liduke aliongeza “Safari hii tumeingia kwenye kilimo kwasababu kwa Njombe ni uti wa mgongo lakini wakulima wamekuwa na kilimo cha mazoea,na tunachohitaji watu walime kilimo bora chenye ufanisi na kitakacholeta matokeo chanya kwa mkulima”aliongeza Bi,Liduke


Nolasco Kilumile ni afisa wa mazao kutoka halmashauri ya mji wa Njombe (HQ).Amesema mashirika mengi yanakuja kwa mgongo wa  NGO's lakini wanafanya biashara hivyo amewataka wakulima kukopa kwa hiari yao huku akiwataka kujenga mitaji yao wenyewe.



Vile vile amesema wanaendelea kuyafuatilia mashirika yanayofanya kazi kwa mwamvuli wa  NGO's wakati yanatafuta faida kwa kutoa mikopo mibaya na ya kuumiza wakulima.


“Haya mashirika tunaendelea kuyafuatilia,yale yenye mikopo mibaya lazima tuyafutilie kama tulivyofanya kwa moja ya shirika siwezi kulitaja hapa,lazima tuhoji kwa mwamvuli wa NGO's inakuwaje wewe utafute faida”alisema Nolasco Kilumile


Post a Comment

0 Comments