TANGAZA NASI

header ads

Tari Uyole yakoshwa na wakulima wa Njombe ni baada ya kufuata kanuni za kilimo

 




Na Amiri Kilagalila,Njombe


Serikali kupitia kituo cha utafiti wa kilimo nchini  kanda ya kusini Tari Uyole imewataka wakulima kuendelea kuzingatia kanuni bora za kilimo wanazoelekezwa na wataalamu ikiwa ni pamoja na kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti kulingana na vipimo vya udongo katika maeneo yao.


Mkurugenzi wa kituo Dkt, Tulole  Lugendo Bucheyeki ametoa kauli hiyo alipotembelea mashamba ya wakulima katika kijiji cha Ilunda wilayani Njombe na kufurahishwa na mwenendo wa wakulima ambapo amesema maendeleo makubwa yanaonekana kwa wakulima baada ya kupewa elimu ya utalaamu wa kilimo pamoja na matumizi ya mbegu zinazofanyiwa utafiti na kituo cha utafiti.


“Hapa Ilunda nimefurahishwa kweli kweli,lakini kuna baadhi ya wakulima ambao hawatumii tekinolojia ambazo tunawafundisha tunaamini hawawezi wakatumia tekinolojia hiyo kwa mwaka mmoja.Tuna mbinu nyingi za kuendelea kuhaulisha hizo tekinolojia na tutaendelea kuwafundisha zaidi”alisema Dkt,Bucheyeki


Nickson Mbogela  ni mmoja wa wakulima wa mahindi na viazi mazao mengine mbali mbali aliyetembelewa katika kijiji cha Ilunda,amesema ujuzi alioupata kupitia kituo cha utafiti kwenye zao la mahindi na Viazi umemsaidi kupata mazao yenye tija na kuiwezesha familia yake kiuchumi.


“Ninalima mahindi na viazi kwa kweli elimu imenisaidia sana kupata mazao bora na ninavuna mazao mengi yanayoniwezesha katika chakula na nikiuza basi naweza kupeleka watoto shule nimejenga nyumba lakini pia hadi nimeweza kununua Ng’ombe na Nguluwe”alisema Nickson Mbogela


Naye Milton Myava ni mkulima wa parachichi katika kijiji hicho aliyetembelewa na mkurugenzi amesema kupitia mashamba darasa imekuwa msaada mkubwa kwao katika kulima na kuzalisha kwa tija kwani amefanikiwa kuboresha kilimo chake ukilinganisha na hapo awali walipokuwa wanalima kilimo cha mazoea.


“Tulikuwa hatujui kama parachichi itakuwa ni biashara au ikatupatia kipato lakini ndani ya miaka mitatu mimi nilivuna na kwa kweli kupitia Tari nimeweza kugundua parachichi  ni zao la biashara ambalo lipo vizuri”Alisema Myava


Kwa upande wake afisa kilimo wa kijiji cha Ilunda bwana Disbord Ntila amesema wamekuwa wakiendelea kuwaelekeza wakulima namna ya kuzingatia kulima kitaalamu hatua ambayo imekuwa ikiwasaidia sana katika maisha yao licha ya kuwapo kwa baadhi ya changamoto zikiwemo gharama kubwa za pembejeo pamoja na kukosekana kwa mtaji wa kutosha.


“Mara nyingi tunapenda kutoa wito kwa wakulima wanapopata elimu kwenye mashamba darasa isiishie tu kichwani na kwenye madaftari inafaa ikatumike shamabani kama wanavyofanya baadhi na ndio elimu inayofaa ili tuweze kufanikiwa”alisema Disbord Ntila

Post a Comment

0 Comments