TANGAZA NASI

header ads

Changamoto za elimu Ludewa zamfikia mbunge aahidi kutafuta ufumbuzi

 



Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ameahidi kununua vitabu kwa shule za msingi zilizopo jimboni kwake baada ya kupewa taarifa kuwa wanafunzi wanamaliza shule bila kutumia vitabu vya masomo mbalimbali vya mitaala mipya ili kukuza kiwango cha elimu.


Ahadi hiyo ameitoa alipokutana na walimu wakuu wa shule za misingi zilizopo jimboni kwake na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za kielimu ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi na kukuza kiwango Cha elimu wilayani humo.


Wakiwa katika mkutano huo walimu walieleza changamoto nyingi zinazowakabili na kupelekea kushika nafasi ya mwisho ikiwemo kutokuwa na vitabu vya kufundishia, wazazi kuwashawishi watoto kufanya vibaya mitihani yao ya mwisho, utoro kwa wanafunzi na nyinginezo.


Suzana Kibena ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nkau ambaye alinieleza mbunge huyo changamoto hiyo ya vitabu na kudai kuwa kwa miaka mitatu sasa mfululizo darasa la nne na la saba wamekuwa wakifanya mitihani ya taifa kwa kusoma bila kutumia kitabu Cha sayansi.


Alisema serikali imekuwa ikiwasisitiza kupakua vitabu hivyo mitandaoni kitu ambacho kwa upande wao inawawia vigumu kutokana na kufanya hivyo kunahitaji gharama na wao hawana fedha za kupakulia vitabu hivyo.


"Tunaambiwa tupakue vitabu mtandaoni na kuvitumia kwa wanafunzi ilihali vitendea kazi hatuna,Kama kopyuta, printer na vinginevyo na ukisema uende stationary nako kunahitajika hela ya kufanya hivyo, sisi tunaitoa wapi? ", Alisema Kibena.


Akizungumza baada ya kusikiliza changamoto hizo mbunge huyo alisema yeye pamoja na mwenyekiti wa halmashauri Wise Mgina  watashirikiana na walimu hao katika kutatua changamoto hizo na kuweka mkazo katika suala la kutokuwepo kwa  vitabu ambapo aliahidi kununua vitabu hivyo huku akimtaka afisa elimu wa wilaya hiyo Daniel John kutatua tatizo hilo kwa muda kwa kupakua mtandaoni vitabu hivyo na kuchapisha ili wanafunzi waanze kutumia wakati wakisubiri ufumbuzi wa kudumu.


"Changamoto zenu nimezipokea na ninaahidi kushirikiana nanyi katika kuzitatua ili muweze kufundishia katika mazingira mazuri na watoto wa wapiga kura wangu waweze kupata elimu bora na itakayowawezesha kufanya vizuri na kukuza kiwango cha elimu wilayani kwetu", alisema Kamonga.


Naye afisa elimu wa shule za msingi wilayani humo Daniel John kwa niaba ya walimu wakuu hao amemshukuru mbunge huyo na kumuomba kuendeleza ushirikiano huo ambao unaweza kuleta matoke chanya katika sekta ya elimu.


Sanjari na Shukrani hizo afisa huyo alimuomba mbunge huyo kuzungumza na wananchi wake waache vitendo vya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha walimu kwakuwa walimu hao wanafanya kazi kubwa sana ya kuwafundisha watoto wao.


"Nazungumza haya kwa uchungu Sana! kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwazalilisha walimu wangu na kuwanyanyasa pasipo sababu ya msingi, walimu tunawafundisha watoto wao katika mazingira magumu halafu bado na wazazi wanatuongezea matatizo, tafadhari sana Mheshimiwa mbunge naomba uzungumze na wananchi wako waache kuninyanyasia walimu wangu", Alisema afisa elimu huyo.


Aidha kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama Cha walimu (CWT) mkoa wa Njombe Shabani Ambindwile akimuwakilisha katibu mkuu CWT taifa amewasisitiza walimu wakuu hao kuwa na ushirikiano na walimu wao na kujenga upendo kati yao ili kuhakikisha shule zao zinafanya vyema.


Alisema pamoja na kujenga upendo kati yao pia wanapaswa kutowavumilia walimu wazembe kwani kutokana na uzembe wao nipelekea kuleta matokeo hasi katika shule zao halafu yanapikuja matokeo mabaya analaumiwa mwalimu mkuu.


"Mimi wakati nafundisha nikiona mwalimu mzembe nilikuwa namtupa kwenye stadi za kazi huko kutamfanya ajifunze na kuongeza juhudi katika kufundishia, japo sina maana nanyi mkafanye hivi Ila hakikisheni hamuwafumbii macho walimu wa aina hiyo", alisema Ambindwile.


Naye mmoja wa walimu wakuu hao aliyefahamika kwa jina la John Kayombo ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lusitu iliyopo kata ya Madope alisema ili shule hizo ziweze kufanya vizuri viongozi wa serikali wanapaswa kuwasomesha watoto wao katika shule za kawaida ambazo na watoto wa masikini wanasoma kwani itasaidia kuondoa changamoto mbalimbali za kielimu.


" Endapo viongozi watawasomesha watoto wao katika shule hizi basi watafanya juhudi kuhakikisha shule zinakuwa na vitabu vya kutosha na vitu vingine ili watoto wao waweze kupata elimu iliyo bora lakini bila hivyo watoto wa masikini ndio wataendelea kuteseka na changamoto hazitaweza kumalizika", alisema Kayombo.

Post a Comment

0 Comments