Urusi inasema moja ya meli ya zake za kivita imepata meli ya kivita ya Marekani imeingia kwenye eneo lake la maji na kuanza kuifukuza katika Bahari ya Japani Jumanne.
Urusi imeshtumu meli hiyo ya Marekani ya USS John S McCain kwa kusafiri zaidi ya kilomita 2 kutoka eneo la mpaka na kusema ilitaka kuilipua meli hiyo.
Baada ya kufuzwa, meli hiyo ya kivita ya Marekani iliondoka eneo hilo, kulingana na taarifa kutoka Urusi.
Hata hivyo, jeshi la majini la Marekani limekanusha kufanya makosa yoyote na kusema meli yake "haijakatazwa" kufika eneo hilo.
Tukio hilo lilitokea Jumanne katika Bahari ya Japan, ambayo pia inafahamika kama Bahari ya Mashariki, eneo la maji linalopakana na Japani, Urusi na Korea zote mbili.
Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Urusi, meli yake ya kivita ya Admiral Vinogradov iliwasiliana katika ngazi ya kimataifa kutoa onyo kwa meli za Marekani juu ya "uwezekano wa kulipua meli husika kwa kuingia katika eneo lake la maji".
"Taarifa ya Serikali ya Urusi ni ya uongo," amesema msemaji wa jeshi la Marekani nchni Japani, Luteni Joe Keiley. "Meli ya USS John S McCain 'haikukatazwa' kuingia eneo hilo na taifa lolote lile."
Msemaji huyo aliongeza kuwa Marekani haitawahi kutishika au kushinikizwa kukubali madai ya uongo kuhusu masuala ya majini kama yaliyotolewa na serikali ya Urusi.
Matukio kama hayo baharini ni nadra sana kutokea ingawa meli nyingine ya kivita ya Urusi ya Admiral Vinogradov iliwahi kuhusika na tukio la aina na meli ya kivita ya Marekani katika Bahari ya China Kusini mwaka jana.
Nchi zote mbili Marekani na Urusi zililaumiana kwa tukio hilo.
Nchi hizo mbili mara nyingi hushtumiana kwa kuingiliana vibaya katika matukio ya kijeshi ama iwe baharini au kwenye anga.
Mwaka 1988, meli ya kivita ya Usovieti ya Bezzavetny, ilikwaruza meli ya kivita ya Marekani ya Yorktown katika Bahari Nyeusi, kwa kuishtumu kwa kuingia kwenye eneo lake la maji.
Uhusiano kati ya Urusi na Marekani haujaimarika na Rais Vladimir Putin bado hajampongeza Rais mteule Joe Biden kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Marekani uliofanyika Novemba 3.
Nchi hizo mbili bado hazijakamilisha makubaliano ya mwisho ya silaha za nyuklia kati yao ambao utafikia ukomo wake Februari.
Mwaka 2017, meli hiyo ya kivita ya Marekani ya USS John S McCain ilihusika katika mgongano na meli ya mafuta ya Singapore, huku mabaharia 10 wakiuawa.
0 Comments