Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, Dk. Tulia Ackson, ameanza utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi, ambapo kila Alhamisi atakuwa anasikiliza kero mbalimbali katika ofisi yake iliyoko kwa mkuu wa wilaya ya Mbeya na kila Jumamosi atakuwa kwenye ofisi zake zilizopo Uyole.
Dkt. Tulia ameitoa hii leo Novemba 23, 2020, wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, na kusema kuwa hiyo ni moja ya ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni kwamba atahakikisha anatenga muda wa kukutana mwananchi mmoja mmoja ili asikilize kero zake.
"Nimeanza utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi wangu kila mwenye shida yeyote afike kwa kulingana na siku nilizozianisha," amesema Dkt. Tulia.
Akizungumzia suala la kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu, Dk. Tulia, amesema kuwa hakuna chochote kilichofanyika kati yake na mtangulizi wake huyo aliyekuwa anatumia Ofisi za Ardhi.
"Hadi sasa hakuna makabidhiano na mbunge mstaafu, Joseph Mbilinyi, siwezi kumlazimisha, mimi nimejiandaa kikamilifu kuwatumikia wananchi siwezi kusubiri kwa sababu naona hajihusishi na chochote na ni mlolongo mrefu, ndiyo maana hata ofisi natumia nyingine", ameongeza Dkt.Tulia.
0 Comments