MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT-Wazalendo Maalim Seif
Sharif Hamad amesema endapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi,
atahakikisha anafanya mambo mengi ya kimaendeleo ikiwemo kujenga
bandari kubwa ya kisasa Unguja na Pemba.

Akizungumza na wananchi wa chama hicho katika Uwanja wa Tibirinzi
Chake Chake kwenye uzinduzi wa kampeni alisema kuwa, kupitia bandari
hizo kutaruhusu makontena kuja moja kwa moja kisiwani Pemba, jambo
ambalo litasaidia kupunguza gharama kwa wananchi.

Alisema kuwa, ataifanya Zanzibar kuwa kituo kikubwa cha biashara kwa
kujenga bandari kubwa itakayosaidia kukuza uchumi na kipato kwa
wananchi kitakachopelekea kupungua kwa umasikini.

“Nitajenga bandari kubwa na ya kisasa Unguja na Pemba, ili makontena
yaje moja kwa moja kisiwani hapa, hii itasaidia vitu kuwa rahisi
ambavyo watamudu kununua hata wananchi wa kipato cha chini”, alisema
Maalim Seif.

Aliwaeleza wananchi kuwa, waakimpa ridhaa ya kuongoza atahakikisha
kila mmoja anakuwa sawa mbele ya sheria, usalama wa raia na kulindwa.

“Mutakaponipa ridhaa nitahakikisha mnakuwa sawa mbele ya sheria na
tutalinda haki za wananchi wote na mali zao”, alisema.

Aliwataka wananchi hao kwenda kwenye vituo vyao vya kupigia kura
ifikapo Oktoba 28, kwani ni haki yao kikatiba na kisheria.

Aidha aliwaahidi wananchi kwamba endapo watampatia ridhaa ya
kuwaongoza atahakikisha baada ya miaka mitano vijana wote wanapata
ajira, ili waweze kujikimu kimaisha.

“Vijana wengi hawajaoa kutokana na uwezo wao kuwa ni mdogo lakini
mutakaponichaguwa, ndani ya miaka mitano nitawapatia ajira ili
mujikwamue kiuchumi mpate kuwaowa akina dada ambao hawajaolewa”,
alisema.

Aidha mgombea huo alisema, ataweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili
kuwavutia wawekezaji, jambo ambalo litasaidia vijana kupata ajira na
Taifa kupata maendeleo.

Kiongozi mkuu wa chama hicho Zitto Zubeir Kabwe alisema kuwa, hakuna
mwananchi atakaezuiwa kupiga kura, hivyo itakapofika siku mwende
mkachague viongozi mnaowataka.

Alisema kuwa, pia chama hicho kitaboresha maisha ya wazazibari, ili
kuhakikisha ufukara na umasikini unaondoka katika visiwa vya Zanzibar
na kuwa nchi ya kimaendeleo.

Nae Makamo Mwenyekiti wa Kampeni  wa  ACT-Wazalendo Mansour Yussuf
Himid alisema wanahitaji kiongozi jasiri, asieyumba na anaeweza
kufanya kazi, hivyo aliwaomba wananchi wamchague mgombea huyo.

Uchaguzi mkuu wa Zanzibar unatarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu,
ambapo kampeni hizo zinaendelea kesho katika kiwanja cha Polisi Konde
kunadi sera zao.