TANGAZA NASI

header ads

DC Ndemanga awataka wakurugenzi na maofisa maendeleo wasome taarifa za asasi na mashirika yasiyo ya kiserikali



Na Ahmad Mmow, Lindi.


Wakurugenzi watendaji wa halmashauri na maofisa maendeleo ya jamii mkoani Lindi wamehimizwa wasome ripoti za mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia.

Wito huo umetolewa leo na mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga wakati wa  uzinduzi wa ripoti ya tathimini ya mradi wa kuboresha huduma za msaada wa kisheria. Hafla ambayo imefanyika katika manispaa ya Lindi katika ukumbi wa mikutano wa Sea view.

Ndemanga  ambae alizindua ripoti  hiyo kwaniaba  ya mkuu wa mkoa wa Lindi alisema uzoefu unaonesha baadhi ya wakurugenzi, maofisa maendeleo ya jamii na maofisa wa taasisi nyingine za serikali hawasomi ripoti za mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia.

Alisema hali hiyo inasababisha washindwe kujua taarifa muhimu za mashirika na taasisi hizo. Kwahiyo sio jambo la kushangaza kuona na kusikia wakishindwa kujibu maswali muhimu yanayohusu mashirika na asasi hizo ambazo kimsingi ni msaada mkubwa kwa serikali.

Mkuu huyo wa wilaya ya Lindi alibainisha kwamba ndani ya taarifa hizo kuna mambo mengi mazuri ambayo ni msaada kwao katika utekelezaji wa majukumu.

'' Mimi mwenyewe nilikuwepo kwenye NGO' ( Mashirika yasiyo ya kiserikali). Kwahiyo nazijua changamoto zilizopo kwenye NGO'S na asasi za kiraia,'' Ndemanga alitoa ushuhuda,''.

Mbali na hilo la kuwahimiza wakurugenzi na maofisa maendeleo ya jamii, Ndemanga  alitoa wito kwa watekelezaji wa mradi huo uliotekelezwa kwa muda wa miaka minne (2016-2020) na kugharimu takribani shilingi bilioni moja, ambao ni shirika la msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto wa Lindi( LIWOPAC) liendelee kuyasaidia makundi maalumu ya kijamii kutambua haki zake za msingi.

Alisema wazee, walemavu, wanawake na watoto wanahitaji sana msaada wa wasaidizi wa kisheria. Kwani ni makundi yanayodhulumiwa sana haki zake.

Alilihimiza shirika hilo lisambaze taarifa zake kwa wadau mbalimbali ili wasome nakusaidia kufikisha elimu kwa jamii na wajue kwa kina kazi zinafanywa na shirika hilo. Huku akiyataka mashirika na asasi za kiraia kuendeleza miradi pindi wafadhili wanapokoma kufadhili.

Kwaupande wake mkurugenzi wa LIWOPAC, Cosma Bulu alisema ingawa wanawake ni walengwa katika miradi mingi inayotekelezwa na shirika hilo, lakini hawana tabia ya kufuatilia na kusikiliza matangazo na taarifa zinazotolewa na shirika hilo. Kwahiyo ni miongoni mwa changamoto.

Alisema shirika linajitahidi kufikisha ujumbe kwakutumia vyombo vya habari. Hatahivyo wamekuwa wagumu kusikiliza redio, kusoma magazeti, televisheni na mitandao ya kijamii. Kwahiyo alitoa wito wajenge utamaduni wakusikiliza, kusoma na kutazama taarifa.

Mradi wa kuboresha huduma za msaada wa kisheria ulioanza kutekelezwa mwaka 2016 kwa ufadhili wa shirika la kusaidia mashirika na asasi za kiraia zinazotoa huduma za msaada wa kisheria (LSF) ulikuwa unatekelezwa katika baadhi ya halmashauri zilizopo katika mikoa ya Lindi na Mtwara.


 

Post a Comment

0 Comments