Uturuki na Urusi Alhamis zilikubaliana kuendelea kushinikiza usitishwaji wa mapigano Libya ingawa Uturuki inasema Khalifa Haftar, haaminiki na anastahili kuondoka maeneo muhimu ndipo kuweze kupatikana makubaliano.
Mshauri mkuu wa usalama wa Rais Erdogan Ibrahim Kalin amesema kwa makubaliano yoyote kufanyika, ni sharti vikosi vya Khaftar viondoke katika mji wa Sirte ambao ni lango kuu la visima vya mafuta Libya na uwanja wa ndege wa kijeshi wa Jufra ulioko katikati mwa nchi hiyo.
Kuna mvutano mkubwa kwa sasa kati ya nchi zinazounga mkono pande tofauti Libya
Kulingana na taarifa hiyo ujumbe wa Uturuki na Urusi utatafakari kubuni kundi moja la kiufanyia kazi kuhusiana na Libya na wamepangiwa kufanya majadiliano zaidi mjini Moscow katika siku za hivi karibuni.
Mkutano huu kati ya Urusi na Uturuki unakuja wakati ambapo kuna mvutano mkubwa kati ya nchi zinazounga mkono pande tofauti katika vita hivyo. Ni wiki hii tu ndipo bunge la Misri lilipitisha kutumwa kwa majeshi nje ya nchi hiyo hatua inayotishia kuchochea vita hivyo na kuzileta Misri na Uturuki katika makabiliano ya moja kwa moja. Ibrahim Kalin anazungumzia hali hiyo.
"Misri kufikiria kutuma majeshi Libya haitosaidia smchakato wa kisiasa hasa wakati ambapo sote tunafanya juhudi za kusitishwa kwa mapigano na kujaribu kuusogeza mchakato wa kisiasa upande huo. Nafikiri litakuwa jambo hatari la kijeshi kwa Misri kufanya," alisema Kalin.
Haftar hatotii usitishwaji wa mapigano Libya
Marekani imesema Urusi imetuma ndege za kivita katika uwanja wa ndege wa Jufra ili kuwasaidia mamluki wa Urusi ambao wanapigana pamoja na jeshi la Haftar. Urusi na jeshi la LNA lake Haftar wote wamekanusha haya.
0 Comments