Na Ahmad Mmow, Lindi.
Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini, Selemani Bungara (Bwege) amemuasa kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe atende haki na awe mkweli kwa watu anaowaongoza ili alinde heshima yake na chama kiweze kuaminiwa.
Bwege ameyasema hayo kwenye mkutano wa ndani uliofanyika leo manispaa ya Lindi katika ukumbi wa mikutano wa mtakàtifu Andrea Kagwa.
Bwege alisema miongoni mwa sababu za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kushuka hadhi na vyama wanavyoongoza kushindwa kuaminiwa ni kutokuwa wakweli, wasiotenda haki na kudharau wanachama.
Alisema dharau kwa wanachama na ubabaishaji nitatizo linalosababisha wanachama na wananchi kushindwa kuviamini vyama Wanavyo ongoza na wao wenyewe kupoteza hadhi na heshima.
" Ukiwadharau nawao watakudharau, ukiwathamini, nawao watakuthamini. Usiwaone hivi hawa, wana akili kama mchwa," alisema Bwege.
Bwege alimpa matumaini Zitto kwakumuambia iwapo atawaheshimu na kuwathamini wanachama na wananchi na kutenda haki atakiwezesha chama hicho kuwa na ngome imara katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Katika mkutano huo waliokuwa madiwani wa Chama Cha Wananchi-CUF wa kata nne na kiti maalumu wamejiunga na ACT-Wazalendo na kupewa kadi na kiongozi mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.
Madiwani waliojiunga na ACT-Wazelendo ni Issa Luono, Hawa Kipara, Said Mateva, Ahmad Zuberi na Said Kitunguli. Huku kikipokea na kutoa kadi kwa wananchi wengine ambao wengi wao walikuwa wanachama wa Chama Cha Wananchi-CUF.
Mbali na hayo, katibu mkuu wa chama hicho Addo Shaibu amesema katika ziara ya kiongozi huyo mkuu wa ACT- Wazalendo katika mikoa ya Lindi, Pwani na Mtwara chama hicho kimeingiza wanachama takribani 400. Kati ya wanachama hao wapya, ni madiwani 22 ambao wamehama kutoka CUF.
0 Comments