Na Amiri kilagalila,Njombe
Baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya
Njombe Kwa Kauli Moja limeazimia
kuwafuta kazi watumishi wawili kwa tuhuma za utoro kazini na kutoa barua
ya onyo kwa wengine watano baada ya kamati ya maadili kufanya uchunguzi wa kina
na kujiridhisha kuwakuta na tuhuma za uzembe zilizowafanya kukiuka taratibu za
manunuzi.
Watumishi waliofutwa kazi ni Patrick Kigola mtendaji
wa kijiji cha mfiliga pamoja na Asma Ally ambaye ni mtabibu ambao wanadaiwa
kukutwa na makosa ya utoro kazini kwa zaidi ya miezi miwili na matumizi ya
fedha za umma huku wengine 7 waliopewa barua ya onyo wakidaiwa kufanya uzembe
na kukiuka taratibu wa manunuzi.
Akitoa taarifa hiyo katika kikao cha baraza maalumu
likiwa na agenda 15 ikiwemo ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitano cha
2019/2020 mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Valentino Hongoli
amesema timu ya uchunguzi kutoka kamati ya maadili imefanya uchunguzi usioacha
shaka na kuamua kuwafuta kazi watendaji wawili na kutoa onyo kali la mwisho
wengine saba.
“baada ya kamati ya maadili kujiridhisha na kamati
ya uchunguzi kwa pamoja imeamua kuwafukuza kazi watumishi hao”alisema Valentino
Hongoli
Akifafanua makosa yaliopelekea baraza kutoa uamuzi
huo mkurugenzi wa halmashauri hiyo Ally
Juma akasema ni utoro uliopindukia na kukiuka sheria na taratibu za manunuzi
hatua ambayo imesababisha hasara serikali.
“Watumishi hawa wawili wamefukuzwa kazi kutokana na
utoro kazini lakini kati ya watumishi watano,wanne ni maafisa ugani na mmoja ni
mhandisi wamepewa onyo kutokana na uzembe na kukiuka taratibu za manunuzi”alisema
Ally Juma
Kituo hiki kimezungumza kwa njia ya simu na Patrick Kigora afisa mtendaji aliyefutwa
kazi na baraza la madiwani ambaye anasema kwa kuwa hana taarifa juu ya suala
hilo hivyo hawezi kuzungumza chochote na anachojua bado ni mtumishi wa
serikali.
“Kimsingi mimi hilo siwezi kulizungumzia mpaka
nipewe barua rasmi,mimi natambua bado ni mtumishi wa serikali kwa hiyo siwezi
kusema chochote kwa sasa”alisema Patrick Kigora
0 Comments