RATIBA ya vikao vya Bunge la 11 imebadilika kwa mara nyingine tena, na sasa Rais Dk. John Magufuli atavunja Bunge Juni 16 badala ya 19 kama ilivyokuwa imetangazwa awali.
Awali ratiba ya mwisho kutolewa na Bunge kabla ya hii ya jana, ilionyesha Rais Dk. Magufuli angevunja Bunge Juni 19.
Ratiba hiyo imebadilika mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Kwa mujibu wa ratiba ya sasa, vikao vitafanyika kuanzia saa tatu asubuhi badala ya saa nane jioni na vitafanyika pia siku ya Jumamosi.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Bunge, ilionyesha pia hotuba ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2020-2021 inatarajiwa kuwasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango leo saa 10 jioni huku asubuhi ikiwasilishwa taarifa ya hali ya uchumi.
Kesho na keshokutwa kutakuwa na mjadala kuhusu hali ya uchumi na bajeti kuu na Juni 15 Bunge litahitimisha mjadala huo ikiwa ni pamoja na kupiga kura.
Ratiba ya awali ilionyesha Bajeti Kuu ya Serikali na hali ya uchumi ingewasilishwa leo na kujadiliwa na wabunge kwa siku tatu na kisha kuhitimishwa Juni 17.
Pia Juni 15 utawasilishwa muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi wa mwaka 2020 (The Appropriation Bill 2020 – hatua zote) na muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2020 (The Finance Bill 2020 – kusomwa mara ya pili, kamati ya Bunge zima na kusomwa mara ya tatu).
Siku hiyo pia kutakuwa na Azimio la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kanuni kuhusu marekebisho ya kanuni za Bunge na Waziri Mkuu anatarajia kuwasilisha hotuba yake.
Taarifa hiyo ilionyesha Juni 16 Rais Dk. Magufuli anatarajiwa kulifunga Bunge.
MABADILIKO
Hivi karibuni Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema bajeti kuu ya Serikali itasomwa leo badala ya Mei 20 kama ilivyokuwa inaonyesha awali.
Ratiba nyingine ambayo ilitoka na kubadilishwa ilionyesha bajeti ingewasilishwa bungeni Mei 20, saa 10 jioni na Rais Magufuli alitarajiwa kufunga Bunge Mei 29.
0 Comments