Na Gabriel Kilamlya,Njombe
Halmashauri ya wilaya ya Njombe imeagizwa
kuwachukulia hatua watendaji wake wanaosababisha kwa hoja za kiukaguzi pamoja
na kutakiwa kuzijibu kwa wakati.
Katibu tawala mkoa
wa Njombe Catalina Revocati kwa niaba ya mkuu wa mkoa ametoa agizo hilo
katika kikao cha baraza maalum la madiwani la kujadili hoja za CAG na kwamba
pamoja na halmashauri hiyo kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo lakini
inapaswa kuzifanyia kazi hoja hizo huku mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri
akielekeza kuwachukulia hatua watendaji wanaozalisha hoja za ukaguzi.
“Ninomba sana baraza litoe maelekezo ili mkurugenzi
aweze kulifanyia kazi hasa swala la hoja kwenye ukusanyaji mapato katika leseni
za biashara ili zisijitokeze tena wakati mwingine”alisema Catalina Revocati
“Watendaji wengi hawakaguliwi zinakuwepo hoja nyingi
za wananchi ambazo wanahitaji majibu na hawapati majibu,oneni namna ya
kuwafundisha na kuwakagua”alisema Ruth Msafiri
Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo akiwemo Julius
Salingwa,Roida Wandelage na Shaib Masasi wanasema pamoja na kuridhia kwa hoja
hizo lakini wanataka hatua stahiki kuchukuliwa kwa watumishi ambao wamezalisha
hoja hizo.
“Ukusanyaji wa hizi kodi imekuwaje watu wanaishi
mpaka wanafika mahali wanashindwa kulipa
kodi mpaka wanatutengenezea hoja,tunaomba ukusanyaji ufanyike maana yake
kututengeneza hoja kwenye halmashauri ni kutuharibia”alisema Roida Wandelage
Valentino Hongoli ni mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Njombe ametumia fursa hiyo kumuelekeza mkurugenzi mtendaji Juma Ally
kuhakikisha anazijibu hoja zilizopo ndani ya uwezo wake haraka iwezekanavyo.
“Mkurugenzi jitahidi pamoja na timu yako kuhakikisha
hoja hizi ambazo zimebaki kufungwa,zinasimamiwa ili kufungwa inavyotakiwa hasa
zile ambazo zipo ndani ya uwezo wetu,zipo nyingine ambazo zipo nje ya uwezo
wetu zinahitaji ufuatiliaji kwa mfano hoja za kuhusu tunahitaji kuajili
watumishi wa kutosha inayotoa ajira ni serikali kuu” alisema Valentino Hongoli
Halmashauri ya wilaya ya Njombe imeendelea kupata
hati safi kila mwaka kwa miaka minne mfululizo huku ikifanikiwa kuvuka lengo la
makusanyo ya ndani katika robo ya tatu
ya mwaka wa fedha.


0 Comments