TANGAZA NASI

header ads

La saba kufanya mitiani ya mwisho Octoba 7-8, kidato cha nne Novemba 23


KUFUATIA Rais Dk John Magufuli jana kutangaza kufungua Shule zote ifikapo Juni 29, leo Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako ametangaza ratiba ya masomo na mitihani kwa ajili ya kukamilisha mwaka wa masomo.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Ndalichako amesema muhula wa kwanza wa masomo utamalizika Agosti 28 mwaka huu na kuanza kwa muhula mpya utakaoishia Desemba 18 mwaka huu.

Prof Ndalichako amesema ili kukamilisha muhtasari wa masomo shule zitalazimika kuongeza saa mbili za masomo kwa siku ili kufidia muda uliopotea ambapo maelekezo ya kuongeza muda huo hayatahusisha madarasa ya awali.

Kuhusu ulipaji wa ada kwa shule ya binafsi, Waziri Ndalichako ameshauri Bodi za shule kukaa kwa pamoja ili kuangalia njia nzuri ambayo haitoumiza wazazi na shule.

Amesema kila mmoja ameona namna ambavyo janga la ugonjwa wa Corona lilivyotikisa hali za kiuchumi za wananchi hivyo kushauri busara itumike bila kuziumiza pande zote mbili.

" Hili la ada nishauri tu Bodi za shule zikae na wazazi na kuangalia ulipaji wa ada bila kuumizana. Lakini nishauri tu kwamba kama Mzazi hajalipa ada ya awamu ya kwanza basi ni vema ailipe lakini pia hautokua uzalendo kama shule zitakataa kuwapokea watoto wa kitanzania kisa tu hajalipa ada," Amesema Prof Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amezungumzia mihula ya wanafunzi wa kidato cha tano ambapo amesema wataripoti shuleni Juni 29 kama ilivyotangazwa na watasoma na kukamilisha muhtasari wa kidato cha tano na mitihani watafanya Julai 24 na wataanza masomo ya kidato cha sita Julai 27 mwaka huu.

Ametangaza pia ratiba za mitihani ambapo mitihani ya Kidato cha Nne itaanza Novemba 23 hadi Desemba 11, Kidato cha Pili itaanza Novemba 9 hadi 20, Darasa la Saba Oktoba 7-8 na Darasa la Nne Novemba 9 hadi 20 mwaka huu.

Waziri Ndalichako pia amezitaka shule zote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya katika kujikinga na ugonjwa wa Corona wawapo shuleni.

Post a Comment

0 Comments