Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Aga Khani jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alilazwa Hospitalini hapo tangu Jumanne tarehe 9 Juni 2020 akitokea Hospitali ya DCMCT Ntyuka jijini Dodoma.
Mbowe alifikishwa DCMCT baada ya kudaiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana akiwa anapandisha ngazi nyumbani kwake Area D Dodoma usiku wa kuamkia Jumanne ya tarehe 9 Juni 2020.
Leo Jumamosi tarehe 13 Juni 2020, Tumain Makene, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, ametoa taarifa kwa umma alisema, Mbowe ameruhusiwa kutoka Hospitalini saa 10:30 jioni.
“Ripoti ya matibabu yake inaonesha ataendelea kupata matibabu na uangalizi wa karibu akiwa nyumbani hadi hali yake itakapoimarika kabisa na kupona,” amesema Makene
“Chama na familia kinapenda kutoa shukrani kwa madaktari, wauguzi, wa DCMC, Dodoma na Aghakhan, Dar es Salaam. Aidha, tunawashukuru madereva, marubani, wauguzi na wote waliosaidia kumsafirisha majeruhi kutoka DCMC hadi Aghakahan,” amesema
Makene amesema, shukran pia ziwaendee baadhi ya wabunge, viongozi wa chama, baadhi ya biongozi wa Serikali, wapenzi, wanachama wa Chadema na Watanzania wote wenye mapenzi mema kwa Salaam, Sala na misaada mbalimbali waliyotoa na kuhudumu kwa kipindi chote tangu Mbowe aliposhambuliwa.
“Shukrani za kipekee ziwafikie Mabalozi wote wa nchi mbalimbali, pamoja na asasi mbalimbali zilizotoa salaam za pole na kulaani shambulio hilo huku wakitaka uchunguzi wa haki na wa haraka ili kuwabaini wahalifu “wasiojulikana” waliohusika na kuwachukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema.
0 Comments