Na Mussa John Mara
Serikali imesema baada ya mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji kukamilika kila mtanzania atatakiwa kuwa na umeme na kwamba ambaye atakaidi amri hiyo atachukuliwa hatua.
Akizungumza katika kijiji cha Hunyari wilayani Bunda mkoa wa Mara, baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa kusambaza umeme vijijini ( REA) kijijini hapo, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amesema kuwa serikali inatumia gharama kubwa sana katika kusambaza umeme nchini hivyo ni lazima wananchi kutumia umeme ili miradi hiyo iweze kuwa na tija.
Dkt Kaleman amesema kuwa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote nchini unatarajiwa kuanza mwezi ujao hadi Desemba mwakani lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata na kutumia umeme jambo ambalo litasaidia kuboresha maisha yao kwavile umeme ni mojawapo ya kichocheo cha maendeleo.
Pia amesema serikali imeandaa mazingira mazuri kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na uwezo wa kuunganisha na kutumia umeme kwa kushusha gharama za kuunganishiwa umeme kutoka Sh 177,000 hadi Sh 27,000 gharama ambazo amesema kuwa anaamini kila mtu anaweza kumudu
Waziri Kaleman alisema wananchi hawana uwezo wa kulipa gharama ambazo serikali inatumia kwaajil ya miradi ya umeme nchini huku akitolea mfano mkoa wa Mara ambao hadi sasa serikali imetumia zaidiya Tsh35 bilioni kwaajili ya miradi ya umeme hivyo wananchi wanatakiwa kutumia umeme huo kwajaili ya kujieletea maendeleo.
Amewataka watendaji wa shirika la usambazaji umeme kuhakikisha kuwa kila mtu anayeomba kuunganishiwa umeme apate kwa muda muafaka bila kisingizio chochote huku akisema kuwa kigezo mojawapo ya mameneja wa Tanesco kuendelea na nyadhifa zao ni namna amnavyo wanaongeza idadi ya wateja wanaotumia umeme.
Katika hatu nyingine waziri amesema kuwa serikali haitaongeza muda kwa wakandarasi wanaotekelekeza mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa Kwanza ambao unatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na kwamba mkandarasi atakayeshindwa kukamilisha kwa wakati atachukuliwa hatua kwa mujibu wa mkataba.
0 Comments