Na Ahmad Mmow, Lindi.
Mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amewapiga marufuku waganga wasio na leseni na wapiga ramli chonganishi wanaofanya shughuli zao katika wilaya hiyo.
Ndemanga alitoa agizo hilo jana katika kata ya Chikonji, manispaa ya Lindi baada ya kukabidhi nyaraka za viwanja viwili vya baadhi ya mitaa na shillingi 3.7 milioni ambazo ziliporwa na wajumbe wa mradi wa trekta. Wakati viwanja hivyo viwili viliuzwa na waliokuwa watendaji na viongozi wa mitaa hiyo kinyume cha sheria.
Mkuu huyo wa wilaya ya Lindi alisema katika msimu huu wa mauzo ya ufuta waganga wa jadi matapeli wameanza kuingia wilayani humo kuwatapeli, kuwatia hofu na kuwatuhumu baadhi ya wananchi kuwa ni wachawi. Huku waganga hao wakidai wanatoa uchawi na kuwafichua wachawi.
Aliweka wazi kwamba tabia na vitendo vya waganga hao vinasababisha chuki na mifarakano miongoni mwa jamii. Hali ambayo pia inadhoofisha umoja na mshikamano wa wananchi. Huku akibainisha kuwa waathirika wakubwa wa vitendo vya matapeli hao ni wazee.
Kwakuzingatia ukweli huo, Ndemanga alisema katika wilaya hiyo ni marufuku kufanya kazi ya uganga bila leseni. Pia hataki waganga wanaopiga ramli chonganishi.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Lindi aliwataka waganga hao ambao aliwaita matapeli waondoke na warudi walikotoka.
" Wanatengeneza vitu ambavyo hata mtu mmoja hawezi kukaa. Lakini wanawadanganya watu kwamba hiyo ni ndege ya wachawi yenye uwezo wa kubeba na kusafirisha watu miatano ambayo imeanguka kutoka angani. Nawataka waondoke haraka," Ndemanga alisisitiza.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa vijiji na mitaa waorodheshe mali zote za mitaa na vijiji wanayofanyia kazi na kuwasomea wananchi ili wananchi hao wazijue na waweze kuhoji iwapo hawataridhishwa na taarifa watakazosomewa.
Alisema amebaini kwamba baadhi ya vijiji na mitaa inakusanya fedha nyingi zinazotokana na vyanzo vyake vya mapato. Hatahivyo matumizi ya fedha hizo hayaeleweki, na vijiji na mitaa hiyo hainufaiki.
" Ukienda kukagua unakuta wamefoji matumizi. Eti nauli na posho za safari za kwenda na kurudi ofisini kwa mkuu wa wilaya wakati hawajawahi kuja ofisini kwangu," alisema Ndemanga.
0 Comments