CCM wataka mwanachama atakaye kutwa na rushwa akamatwe hadharani
Na Amiri kilagalila,Njombe
Chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kimeielekeza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU kuwakamata hadharani na kuwachukulia hatua wanachma wa Chama hicho wanaochafua taswira ya Chama kwa kutumia rushwa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Mbele ya vyombo vya habari katibu wa siasa na uenezi CCM mkoa wa Njombe ndugu Erasto Ngole amesema kwa mujibu wa maelekezo ya vikao vya chama hakuna mwanasiasa ndani ya chama hicho atakayesalimika katika mchakato huo kwa kutoa rushwa wala kuandaa makundi ya kukirubuni Chama kwani kinazo taarifa za baadhi ya wanasiasa wa CCM walioanza kujitokeza wakitoa rushwa
“Tunaielekeza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa,tungetamani katika mkoa wetu wa Njombe hawa wanaccm wanatuchafua wangekamatwa mchana hadharani au usiku na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kama watuhumiwa wengine”alisema Ngole
“Halmashauri kuu ya CCM ya mkoa imetoa maelekezo kwamba wale wote ambao tumeshabaini wanapita mitaani na kutoa rushwa,hakuna atakayepenya,hakuna atakayeteuliwa”alisema tena Ngole
Aidha Ngole amesema kuwa kila mwanachama baada ya kipyengwa kupulizwa hapo julai 17 mwaka huu atakuwa na haki ya kuchukua fomu kugombea nafasi yoyote lakini anapaswa kujitathimini kabla ya kuchukua fomu hizo.
Kwa upande wake katibu wa umoja wa vijana wa ccm (UVCCM) mkoa wa Njombe bwana Amos Kusakula amesema vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwani wanayo nafasi kubwa badala ya kudhani kuwa wanatengwa.
“Kwa wa takwimu za sense za mwaka 2012 Inaonekana zaidi ya asilimia 70 ni vijana,sasa kijana lazima ujitambue na uwe tayari kwa kuwa vijana ni muda wao na wanatakiwa kuonyesha uwezo wao na vipaji vyao”alisema Kusakula
Wananchi mkoani Njombe wanazungumziaje vitendo vya rushwa katika chaguzi mbalimbali.
“Kwa kweli wagombea wanaopita na kutoa rushwa kwa ajili ya kuchaguliwa hao hawako sahihi kwasababu anakuwa hajiamini,shida ni kwamba wagombea wengi huwa hawajitambui”Alisema Telesia Mgina Mkazi wa Njombe mjini
Mwezi Oktoba mwaka huu serikali ya Tanzania inatarajia kuendesha zoezi la uchaguzi mkuu wa kuwapata viongozi watakaohuduma nafasi ya Udiwani,Ubunge na Rais katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
0 Comments