Serikali kupitia Wizara ya Nishati na kwa kushirikiana na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ipo mbioni kuhakikisha Vijiji vyote 141 Mkoani Kagera vinapata huduma ya Nishati ya Umeme ndani ya siku chache kuanzia sasa hii ni kutokana na Mradi huu wa usambazaji Umeme Vijijini Mkoani Kagera kuendelea Vizuri.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutembelea Kijiji cha Kyamalange kilichopo Tarafa Bugabo, na kujionea jinsi mradi huo unavyoendelea Mhandisi Jones F. Olotu amabae pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kiufundi kutoka REA, amefafanua kuwa Mradi huo wenye thamani ya pesa ya Kitanzania Sh. Bilioni 51 unaotekelezwa na Mkandarasi NAKUROI INVESTMENT COMPANY LTD yenye Makao yake Makuu Jijini Dar es Salaam, kwa sasa upo katika hatua za mwisho Wa ukamilishwaji, ikiwa umefikia Asilimia 95 za ujenzi wa mradi huo, na kwamba kufikia Tarehe 31 Juni mkadarasi atatakiwa kukabidhi mradi huo kwa mujibu wa mkataba.
"..mradi huu kimsingi unapaswa kukamilika Tarehe 30 Mwezi wa Sita, kwahiyo tunafanya ziara kuweza kukagua kujua mkandarasi amefikia wapi, nini kimebakia na changamoto gani na namna gani tunaweza kuzitatua kabla ya kufika ukomo wa mradi na kuanza kuwekeana penati za Ukomo wa mkataba..." Amesisisitiza Mhandisi Jones.
Kwa upande wao wasimamizi wa mradi huo TANESCO - Kagera, kupitia kaimu Meneja Mkoa Kagera Mhandisi David Mhando amesema wamejipanga kuendelea kumsimamia mkandarasi pamoja na kuhakikisha uunganishwaji wa Wateja unafanyika kwa Kasi huku elimu ikiendelea kutolewa kwa kiasi kikubwa Mkoa mzima ili wananchi wafahamu utaratibu mzuri wa namna ya kuunganishwa na jinsi ya kulipia huduma.
Sambamba na hayo Mwakilishi kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Edson Ngabo ambae ni msimamizi wa miradi ya REA Kanda ya Ziwa, amekiri mkandarasi kuwa na vifaa vya kutosha isipokuwa tatizo magenge hayatoshi na hivyo kusisitiza mradi huo kukamilika ndani ya muda, vinginevyo Tarehe Mosi Julai wataletwa wakandarasi wengine wapya na yeye atakatwa hela kulingana na mkataba, huku akihimiza wakazi wa Kagera kusuka umeme wa majumba yao (wirering).
Nae Mwakilishi wa Mkandarasi ambae pia ni Meneja mradi Mhandisi James Julius James amekiri kupokea mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi wa mradi huo, na kuahidi kutumia nguvu ya ziada ili kukamilisha mradi kwa wakati, ambapo licha ya changamoto zilijitokeza kulingana na ukubwa wa Mkoa na jiografia ya Mkoa wenyewe, tayari mkandarasi huyo amekwisha washa vijiji 102 huku Vijiji 39 Vikiwa katika hatua za mwisho kuunganishwa.
0 Comments