Na Veronica Mwafisi, MOHA-Morogoro
KATIBU
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Chritopher Kadio, ameitaka
Idara ya Huduma za Uangalizi kuhakikisha wafungwa wenye vifungo vya nje
wanafanya kazi zinazoonekana kwa wadau.
Alisema
kutekelezwa kwa agizo hilo, wadau wataona faida ya wahalifu kutumikia
adhabu zao nje ya Magereza badala ya kufanya usafi kwenye maofisi.
Kadio
aliyasema hayo Mjini Morogoro jana wakati akifungua mkutano wa siku
mbili unaoshirikisha Maafisa Wafawidhi wa idara hiyo kutoka mikoa 23
nchini.
Alitoa
wito kwa idara hiyo kuandaa mpango mkakati ambao utaiwezesha Serikali
kupunguza mzigo wa kuwahudumia wahalifu waliopo gerezani.
Alisema
baadhi ya wahalifu wanaweza kutumikia adhabu zao nje ya Magereza hivyo
ni wakati muafaka kwa idara hiyo kuwa na suluhisho ili changamoto hiyo
iweze kupatiwa ufumbuzi.
“Lipo
tatizo kubwa ambalo linaukabili mpango huu hasa fikra za kizamani kuwa
adhabu ya kila mhalifu ni kwenda jela, dhana ya adhabu mbadala bado
haijakolea katika fikra za wengi.
“Fikra
hizo zipo kwenye sekta zote za jamii yetu kuanzia katika mahakama,
baadhi ya Mahakimu wana kigugumizi cha kutoa adhabu za kutumikia jamii
nje ya jela,” alisema.
Alifafanua
kuwa, pia kwenye jamii vijijini na mitaani bado hawajaona umuhimu wa
kutekeleza jukumu la kuwarekebisha na kuwalea jamaa zao wnaojiingiza
katika uharifu.
Kadio alisema viongozi wa kisasa nao hawajalichangamkia jambo hilo na kulipigia debe kwa nguvu zote.
“Ni
imani yangu kuwa idara pamoja na Wizara tunalo jukumu la kuhamasisha na
kutoa elimu kwa wadau tukianzia mikoani, kila kiongozi wa Mkoa awe na
mpango kazi wa kuelimisha.
“Mbali
ya kuhamasisha matumizi ya adhabu mbadala pia ni jukumu letu
kuhamasisha jamii ijiepushe na vitendo vya uhalifu, kuheshimu utawala wa
sheria unaozingatia haki,” aliongeza.
Alisema
pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili idara hiyo katika utendaji
kazi wao, aliwataka wakuu wa idara watafute ufumbuzi wake badala ya
kuitegemea serikali izitatue.
Kadio alisema Wizara hiyo itaendelea kuwawezesha kadri inavyoweza ndio maana kila mwaka inaboresha bajeti yao.
“Ni
vema mkafahamu kuwa, dhamira na dira ya Wizara yetu ni kudumisha
utulivu, usalama na amani kwa Watanzania na ili dhamira hii ikamilike,
idara imepewa jukumu la kusimamia utekelezwaji wa adhabu mbadala ya
kifungo gerezani.
“Mnalo jukumu la kuchangia mafanikio ya Wizara iweze kufikia dhamira yake kwa Taifa,” alifafanua.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Idara hiyo, Aloyce Musika, alisema lengo la
mkutano huo ni kufanya tathmini ya shughuli zilizofanyika mwaka mzima,
kupanga mipango ya mwaka ujao.
Alimshuruku
Kadio kwa kufungua mkutano huo ambao unashirikisha Maafisa Wafawidhi
kutoka mikoa 23 ambayo wameifikia nchini isipokuwa mikoa mitatu ya
Katavi, Lindi pamoja na Ruvuma.
“Miaka
yote tumekuwa tukifanya mkutano kama huu kwa mafanikio makubwa mbali ya
ugumu wa bajeti lakini Wizara imekuwa karibu na sisi, kukaa pamoja,”
alisema.
0 Comments