TANGAZA NASI

header ads

Njombe:Wananchi wasema CORONA siyo sababu ya kushindwa kuboresha taarifa za mpigakura


Na Maiko Luoga,Njombe

Wananchi mkoani Njombe wamesema hawaoni sababu ya kuwazuia kwenda kujiandikisha na kuboresha Taarifa zao kwenye Daftari la kudumu la mpigakura licha ya uwepo wa mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19).

Baadhi ya Wananchi wa vijiji vya Kiyombo na Mkiu Kata ya Lubonde Wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe akiwemo Bw, Essau Chogo amesema licha ya Uwepo wa Janga la CORONA lakini Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa maelekezo ya kuzingatia ili kila mmoja aweze kuyafuata kwa lengo la kujikinga na Janga hilo.

Dkt, Evaristo Mtitu Mhadhiri wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania Jijini Dar es Laam ambae ni Mzawa wa Kijiji cha Mkiu Wilayani Ludewa amefika Kijijini hapo kuhakiki na kuboresha Taarifa zake kwenye Daftari la Mpigakura amesema Wananchi wanatakiwa kushiriki zoezi hilo kikamilifu huku wakizingatia Maelekezo ya Wizara ya Afya.

Amesema Baada ya kufika Kwenye Kituo cha Uandikishaji Wapigakura amekuta Vifaa vyote vya kujikinga na CORONA vipo ikiwemo Ndoo yenye maji tiririka na Sabuni, Vitakasa Mikono pia Watu wanazingatia kukaa kwa umbali wa mita moja jambo ambalo linahamasisha Wananchi kujitokeza na kushiriki zoezi hilo.

Bw, Germano Mguli na Bi, Christina Kalinga Wakazi wa Mtaa wa Mjimwema Mjini Njombe wakiwa kwenye Kituo cha Uandikishaji Wapigakura katika Shule ya Msingi Mjimwema wamesema, wamejitokeza kuboresha Taarifa zao ili kupata nafasi ya kuchagua Viongozi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika Mwaka huu.

Bi, Verdiana Mnzeru Afisa Mwandikishaji Msaidizi Kata ya Lubonde Wilayani Ludewa na Bw, Augustino Ngailo Afisa Mwandikishaji msaidizi Kata ya Mjimwema Mjini Njombe wamesema, Mahudhurio ya Wananchi wanaoboresha Taarifa zao kwenye Daftari la Mpigakura yanaridhisha licha ya uwepo wa hofu ya Homa ya Mapafu.

Aidha Wamesema kwenye Vituo vyote vya Uandikishaji Vimewekwa Vifaa muhimu vya Kujikinga na Virusi vya CORONA ikiwemo Ndoo zenye Maji Tiririka, Sabuni na Vitakasa Mikono ili Wananchi wanaofika kupata huduma wavitumie kwa lengo la Kujikinga na Virusi hivyo vya CORONA.

Serikali imetoa muda wa siku tatu kuanzia Tarehe mbili hadi nne Mwezi Mei 2020 ili kutoa nafasi kwa Wananchi Mkoani Njombe na Mikoa mingine Nchini kuboresha Taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura mapema kabla ya Uchaguzi Mkuu kufanyika.


Post a Comment

0 Comments