Baraza la habari Tanzania (MCT) limetoa salamu za pole kwa mkurugenzi wa shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk. Ayub Rioba, familia nzima ya televisheni hiyo na wafiwa wote kwa misiba ya wanahabari wake.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga ilieleza kuwa Baraza lipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.

Shirika hilo limepoteza wafanyakazi wake watatu katika kipindi cha wiki moja.

==>>Hapo chini ni Taarifa ya MCT

Baraza la Habari Tanzania (MCT) linatoa salamu za pole kwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dr. Ayub Rioba, familia nzima ya TBC, na wafiwa  wote kwa misiba ya hivi karibuni kituoni hapo. Baraza liko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.

MCT inachukua nafasi hii kuwakumbusha viongozi wa vyombo vya habari, wahariri na wanahabari wote kuzingatia mwongozo tulioutoa hivi karibuni kuhusu kujikinga dhidi ya maambukizo ya virusi vya Corona wakati wakiwa kazini, na jinsi ya kuandika habari za janga hilo kwa weledi.

MCT inasisitiza kuwa janga “limeshaingia chumbani” hivyo ni vyema pale mwanahabari anapojisikia dalili zinazohusiana na maambukizi ya Corona atoe taarifa kwa mhariri wake mara moja na achukue hatua  za tahadhari ikiwemo kutokwenda kazini na kwenda hospitalini au kwenye kituo cha afya mara moja.

Baraza linapenda pia kuwasisitizia viongozi wa vyombo vya habari kuchukua hatua za kuwalinda wafanyakazi wao wote kama inavyoelekezwa na wataalamu wetu.

Tuchukue tahadhari na Mungu atuepushe na madhila zaidi.

Kajubi D. Mukajanga

Katibu Mtendaji