Washington,Marekani.

Mamlaka ya chakula na dawa nchini Marekani (FDA),imeruhusu dawa za chloroquine na hydroxychloroquine kutumika kutibu virusi vya corona (Covid-19).

Taarifa ya idara ya afya na huduma za binadamu nchini humo ilisema dawa hizo zimeruhusiwa baada ya utafiti kuonyesha kuwa zina uwezo wa kutibu virusi vya corona.

Hata hivyo, wanasayansi nchi humo wameonya matumizi ya kupindukia ya dawa hizo yanaweza kusababisha madhara.

Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, Anthony Fauci alisema “inapaswa kuwa waangalifu sana na matumizi ya dawa hizo.”

FDA pia imeruhusu kusambazwa dawa hizo katika hospitali zote nchini humo.

Wiki iliyopita Rais wa Marekani, Donald Trump alikaririwa akisema dawa hizo ni zawadi kutoka kwa Mungu kutokana na uwezo wake wa kutibu virusi vya corona.

Katika hatua nyingine, Rais Trump ameongeza zuio la kutotoka nje kwa wiki mbili zaidi.

Jumatatu iliyopita Rais Trump alitangaza amri ya kutotoka nje kwa siku 14 kwa wakazi wote wa miji iliyoathirika na virusi vya corona zuio ambalo lingeisha kipindi cha Sikukuu ya Pasaka.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter Rais Trump alisema amri hiyo inatokana na virusi hivyo kuendelea kusambaa kwa kasi.

“Idadi ya vifo huenda ikaongezeka katika kipindi cha siku 14 zijazo huku maambukizi mapya yakiisababisha hospitali kuzidiwa,” alisema Trump.

Awali Dk Fauci alisema virusi hivyo visipodhibitiwa vinaweza kusababisha vifo vya watu 200,000. Alisema mpaka jana asubuhi nchi hiyo ilikuwa na zaidi ya watu 140,000 walioambukizwa huku 2,493 kati yao wakipoteza maisha.