Mamia ya watu walishiriki maandamano jana katika miji ya Berlin na Stuttgart nchini Ujerumani kupinga hatua zilizowekwa na serikali kuilinda nchi dhidi ya virusi vya corona.
Karibu waandamanaji 1,000 walikusanyika katika mji mkuu wa Ujerumani wakisema kwa sauti kubwa "Ninataka kurudishiwa maisha yangu" na kubeba mabango yenye ujumbe kama vile "Zilinde haki za kikatiba".
Waandamanaji walisambaza magazeti yanayohoji umuhimu wa hatua za kuwafungia watu majumbani na kudai kuwa virusi vya corona ni jaribio la kunyakua madaraka kwa kueneza hofu.
Ilikuwa ni Jumamosi ya nne mfululizo ya maandamano mjini Berlin.
Mjini Stuttgart, kati ya watu 350 na 500 waliingia mitaani huku kiongozi wao akisema maandamano hayo yalikuwa ya kuunga mkono haki za msingi kama vile uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kuabudu.
Mkusanyiko huo ulikuwa umepigwa marufuku kabla ya kuruhusiwa na Mahakama ya Kikatiba.
0 Comments