Na WAMJW- DSM
Mrakibu mwandamizi wa polisi kanda
maalum ya Dar es Salaam ASP Swebe ametoa wito kwa wananchi, hususan
Wana Dar es Salaam kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya
homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
Ameyasema hayo wakati akiwa katika
majukumu yake ya ukaguzi wa namna gani kituo cha Polisi Pangani
kilichopo Ilala Jijini Dar es Salaam kimechukua hatua ya kukabiliana
dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
“Tunaendelea kukumbusha Wananchi
wa hususan Wanaotoka Jijini Dar es Salaam kunawa mikono na kuchukua
hatua zote za tahadhari zinazotakiwa, tunaendelea kusisitiza kila mmoja
katika familia yake aendelee kuchukua hatua ambazo Wizara ya Afya
inapendekeza” alisema
Kwa upande mwingine, ASP Swebe
ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuja na kampeni ya
“Mikono safi, Tanzania salama” inayohamasisha wananchi kuchukua
tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, hali inayoonesha
jinsi gani Serikali imewekeza kwenye Afya ya wananchi.
“Kwanza nitoe shukrani kwa
Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa Kampeni inayoendelea ya “Mikono
safi, Tanzania salama”, hii inaonesha ni jinsi gani Serikali imewekeza
kwenye Afya ya wananchi” alisema.
Aidha, ameishukuru Wizara ya Afya
kwa kuendelea kulisaidia Jeshi la polisi vifaa vya kujikinga dhidi ya
maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona
ikiwemo vitakasa mikono na Barakoa (mask).
Kwa upande wake, Sfaff sergeant
(S/Sgt ) Valentine Ngowi, amewataka madereva wote wa vyombo vya moto
hususan bodaboda na bajaj kuhakikisha wanavitakasa vyombo vyao vya
usafiri kwa sabuni mara kwa mara ili kuua maambukizi ya virusi vya
Corona endapo vitakuwepo.
Uhamasishaji huu unafanywa kupitia
kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya
Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR
kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre
Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.
0 Comments