TANGAZA NASI

header ads

Madiwani wakomaa na serikali kudhibiti Corona “tumekaa kama hatuna baba”



   

Madiwani wa halmashauri ya mji wa Njombe wakati wakiendelee kufuatilia mjadala wa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Njombe




Diwani wa kata ya mji Mwema Abuu Mtamike akitoa ufafanuzi juu ya matumizi ya kituo kipya cha mabasi Njombe mjini na namna ya kujikinga na Corona




Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri akitoa msimamo wake juu ya matumizi ya vituo vya mabasi Njombe Mjini.

Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Edwirn Mwanzinga akihamasisha madiwani na wananchi kuendelea kujikunga na virusi vya Corona.


Na Amiri kilagalila,Njombe

Madiwani wa halmashauri ya mji wa Njombe,wameitupia lawama serikali ya mkoa huo kwa kuiacha halmashauri bila majibu juu ya kupambana na virusi vya Corona katika halmashauri hiyo inayopokea wageni wengi wanaopita kuelekea mikoa jirani huku wengine wakifika katika stendi ya mji wa Njombe (ya mkoa) kabla ya kuelekea wilaya nyingine.

Madiwani wameibua mjadala mzito wakihitaji majibu stahiki kutoka serikalini juu ya kudhibiti virusi hivyo katika halmashauri ya mji wa Njombe wakati wakichangia hoja za kamati ya afya katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika halmashauri hiyo.

Abuu Mtamike ni diwani wa kata ya mji Mwema huku Siglada Mligo na Angela Mwangeni ni madiwani wa viti maalum wanasema ni kweli serikali imeandaa karantini za wagonjwa lakini bado kituo sahihi cha mabasi hakitumiki ipasavyo ili kuweza kudhibiti virusi vya Corona kwa kuwapima watu wanapoingia na kutoka,badala yake wamekuwa wakishushwa kila eneo jambo ambalo ni hatari na ni gumu kukabiliana na mgeni anayeingia na maambukizi.

“Sisi wananchi wa mkoa wa Njombe au wa halmashauri ya mji wa Njombe tumeachwa,tumekaa kama hatuna baba au mama anayetulea,viongozi wameiacha halmashauri haina majibu,leo hii tulitakiwa tuambiwe mkoa umetoa sapoti gani kuhusu huu ugonjwa,tunalalamika hapa hiki chanzo cha stendi mnachokichezea chezea tuludisha pale kwa kuwa ni sehemu sahihi ya kuwamonita watu wanaongia lakini bado watu wanashuka pale chini lakini kwenye hii stendi pana vitakasa mikono,pana vipima joto na mtu tungemgundua mapema”alisema Abuu Mtamike

Angela Mwangeni ambaye ni diwani wa viti maalum amesema wanaomba kibaki kituo kimoja watu wanaoingia na kutoka waweze kupimwa huku Siglada Mligo akibainisha kuwa baraza hilo la madiwani lilikwisha azmia kuwepo na kituo hicho kimoja lakini mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya awali waliruhusu watu kushuka maeneo ya kituo cha zamani cha mabasi na kuleta shida kudhibiti watu wanaongia na virusi vya Corona kwa kipindi hiki kwa kuwa maeneo mengine hayana huduma za kujikinga.

Naye mwenyekiti wa halmashauri Edwirn Mwanzinga ametoa wito kwa madiwani na wananchi wa halmashauri hiyo kila mmoja kutetea nafsi yake na kuchukua tahadhari dhidi ya virusi hivyo.

“Ninaomba kila mmoja achukue tahadhari ya kwake dhidi ya huu ugonjwa,kuna watu wanataka serikali iseme kuanzia leo magari yasiende Dar es Salaam,tunashida tofauti ukiona wewe shida yako sio ya muhimu sana kuna simu na kila kitu usiende”alisema Mwanzinga

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri amesema ataendelea kusimamia maelekezo ya mkuu wa mkoa badala yake halmashauri iendelee kuchukua tahadhari na kuelimisha watu kuzingatia taratibu za kujikinga na Covid-19.

“Habari ya stendi ya zamani mimi binafsi nitaendelea kusimamia maelekeo ya mkuu wa mkoa,tuchukue tahadhari zile tunazoweza kuchukua tuendelee kuelimisha watu wetu wajue watapandia na kushukia pale kwenye stendi ya zamani lakini kwa kuzingatia taratibu.”alisema Ruth Msafiri

Post a Comment

0 Comments