TANGAZA NASI

header ads

Serikali yazindua muongozo wa utoaji huduma ya chakula na Lishe kwa wanafunzi elimu ya msingi



 Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa  kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project Concern International (PCI) imezindua mwongozo wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimumsingi ili kuondokana na changamoto ya utoro kwa wanafunzi na kuongeza kiwango cha ufaulu.

Akizindua mwongozo huo jijini Dodoma,  uliofadhiliwa  na Serikali ya Marekani kupitia Idara ya Kilimo(USDA), ambao unalenga wazazi na wadau mbalimbali wa elimu kutambua umuhimu wa huduma hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Leonard Akwilapo mebainisha kuwa  takwimu za mwaka 2021 zinaonesha kuna shule 23,835 za elimumsingi zenye wanafunzi 13,708,242, jambo linalochangia umuhimu wa utekelezaji wa mwongozo huo kuwaokoa wanafunzi na utoro na kuongeza ufaulu.

“Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya afya ya mwanafunzi na maendeleo yake kitaaluma, kuna madhara makubwa kwa wanafunzi kukosa chakula shuleni ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa usikivu wakati wa ujifunzaji”. Amesema Dkt Akwilapo.

Ameongeza kuwa “Upatikanaji wa chakula na lishe bora mashuleni utaongeza hali ya wanafunzi kukaa shuleni kwa usikivu na kuwa tayari kujifunza” amesema.

Dkt. Akwilapo amebainisha kuwa  kuwa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inatamka wazi utoaji wa huduma muhimu kama hizo na ni muhimu zikazingatiwa katika shule zote zilizosajiliwa hapa nchini na kuzitaka kila idara za elimu kufuata muongozo huo.

“Utoaji wa huduma umekuwa ukitekelezwa kwa namna na viwango tofauti, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakinufaika sasa serikali imeandaa mwongozo huu wa kisera ili kuleta uratibu wa kitaifa ambao utanufaisha wanafunzi wote wa shule zote nchini,” amesema.

Akizungumzia mwongozo huo amesema utaratibu wa upatikanaji wa chakula, vyanzo vya upatikanaji wa chakula, mifumo ya uchangiaji, aina ya vyakula, mahitaji muhimu, wajibu na majukumu ya watekelezaji, ufuatiliaji na tathmini.

“Nitoe wito kwa wadau wote wa elimu kushiriki kuchangia utoaji wa chakula na lishe kwa kuwa suala hili ni mtambuka linahitaji ushirikiano, ni matumaini yangu kuwa kila mmoja atasoma mwongozo huu na kutekeleza majukumu yote ipasavyo” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa PCI, Nicolas Ford amesema  Shirika hilo lilitekeleza mpango wa chakula kwa elimu Mkoani Mara  ambao umeonesha mafanikio mbalimbali ikiwamo kupunguza utoro na kuboresha mahudhurio kwa asilimia 89 kutoka asilimia 84.5 mwaka 2017.

Ameongeza kuwa  mpango umesaidia kuongezeka kwa uelewa wa wazazi na kuongeza kiwango cha uchangiaji mazao ya chakula hadi kufikia tani 1,662 mnamo Septemba 2021.

Nae Kamishna wa Elimu hapa nchini Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema pamoja na juhudi za serikali za kuboresha miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji hazitatoa matokeo tarajaji kama litasahaulika suala la upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi.

Huku Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Stanslaus Nyongo, amesema Bunge linaunga mkono mwongozo huo na kutoa wito kwa Wabunge na Madiwani kuendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika utoaji wa chakula shuleni

Awali, Mwakilishi wa Balozi wa Marekani hapa nchini , Benjamin Mtaki akitoa maelezo ya Shirika la USDA, amesema Dola za Marekani milioni 67 zimetumika kwa miaka 10 kutekeleza Mpango wa chakula kwa elimu(FFE) ambao ulitekelezwa kwa awamu tangu mwaka 2010.

Post a Comment

0 Comments