TANGAZA NASI

header ads

Uteuzi wa mawaziri wanawake wamkosha mwenyekiti wa UWT Njombe,adai Rais azidi kuonyesha uwiano katika uongozi

 


Na Amiri Kilagalila,Njombe

Mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Njombe Scolastika Kevela amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa mawaziri wapya watatu wakiwemo wanawake wawili hatua aliyodai imeendelea kuleta uwiano wa kijinsia katika uongozi nchini.

Akizungumza na vyombo vya habari Mwenyekiti huyo  ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart alisema uteuzi wa Waziri wa Ulinzi Dkt. Stergomena  Tax pamoja na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji kimeonyesha nia njema ya Rais Samia kuwaheshimisha wanawake. 

Mbali na Mawaziri hao Rais Samia pia alimteua Mbunge wa Bumbuli January Makamba kuwa Waziri wa Nishati na Madini akichukua nafasi ya Dk Medard Kalemani ambaye uteuzi wake pamoja aliyekuwa Waziri Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk Faustine Ndugulile na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Dk Leonard Chamriho, ulitenguliwa.

"Kwa niaba ya wanawake wote wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe tunampongeza Rais Samia kwa uteuzi huu, na zaidi tunatambua jitihada zake za kuhakikisha wanawake wanashika nafasi muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu,nafasi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikishikiliwa na wanaume"alisema Scolastika

Amesema uteuzi huo umeifanya Tanzania kutengeneza historia kwa kuwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye ni mwanamke lakini pia mwanamke wa kwanza kuwa waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Kimsingi uteuzi huo umeongeza nafasi za wanawake mawaziri kufikia 7 sawa na asilimia 30.4 kutoka 5 sawa na asilimia 21.7 huku wanaume wakiwa ni 16 sawa na asilimia 69.6 jambo alilosema ni mwelekeo mzuri katika kufikia idadi ya hamsini kwa hamsini.

"Nitoe wito kwa viongozi wanawake na wanaume waliopo katika nafasi mbalimbali za uteuzi kutumia nafasi zao kikamilifu na kumsaidia Rais ili aweze kutimiza vyema majukumu yake ya kuleta maendeleo endelevu na jumuishi kwa Taifa letu" aliongeza Scolastika 

Alisema akiwa kama Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wa Chama Mapinduzi Mkoa wa Njombe, kwa niaba ya wanawake wote wa Mkoa huo wanamuombe dua njema kwa Mungu ili aendelee kumpa Afya njema ya kuwaongoza watanzania. 


Post a Comment

0 Comments