Siku chache baada ya kuapishwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amekutana na watalaamu wa wizara hiyo na kuwataka kuwalinda wafanyabiashara akisisitiza kuzingatia sheria za ukusanyaji wa mapato na kodi.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo, Dk Nchemba amewataka watumishi wa wizara hiyo na mamlaka zinazosimamia ukusanyaji wa mapato kurekebisha pale ambapo walikosea ikiwa ni pamoja na kurudi kwenye mstari kwa kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria wakizingatia weledi wa kazi yao.
Dk Nchemba amesema ni wakati sasa wa kulinda uchumi wa Taifa letu kwa kuwalinda pia walipa kodi huku akiwataka wafanyabiashara ambao walikua wanaogopa kuweka wazi fedha zao waweke kwenye mabenki kwani serikali itatoza kodi inayostahili na siyo kuchukua fedha za watu.
Amesema Wizara yake itasimamia kwa ukamilifu ukusanyaji wa mapato kama walivyoelekezwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kufuata sheria na taratibu za ukusanyaji wa mapato bila kuathiri uchumi wa Nchi na wa walipa kodi.
" Ili kupata mapato makubwa kwanza ni kukuza uchumi wetu, Rais amesema tulinde uchumi wetu ndio tutapata wigo mpana wa mapato, kila mtu kwenye idara yake ajipange kukuza uchumi wa Nchi yetu lakini kikubwa kama alivyosema Rais Mama Samia tuhakikishe tunaweka mazingira bora ya watu wetu kulipa kodi, tuwatengenezee mazingira mazuri walipa kodi wetu.
Turekebishe pale tulipoenda kinyume, tuache hii ya kuwataka wafanyabiashara walete taarifa zao za miaka 15 iliyopita, turudi kwenye sheria zetu za ukusanyaji mapato tusichukue fedha za watu bali tukusanye kodi kisheria, hii ya kuomba taarifa za miaka ya nyuma tuachane nayo maana kwanza watu wetu hawana utaratibu wa kuhifadhi kumbukumbu, nyie wenyewe nikiwaambia mnipe salary slip zenu za 2005 hamna," Amesema Dk Nchemba.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamadi Masauni amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwateua yeye na Dk Nchemba katika nafasi hizo huku wakiahidi kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato kama ambavyo ameelekeza.
"Nimshukuru Rais kwa kututeua, nimeona tuna timu nzuri ya wataalamu wizarani hapa ambao naamini kwa pamoja tutashirikiana kukuza uchumi wetu na kuweka mazingira bora ya kukuza uchumi wa watu wetu ili waweze kulipa kodi kisheria, lengo likiwa kuiletea Nchi yetu maendeleo kama Ilani ya CCM inavyotuelekeza," Amesema Mhandisi Masauni.
0 Comments