Na Amiri Kilagalila,Njombe


Wakati zao la Parachichi likiteka soko la Dunia na kuwaingizia mamilioni wakulima na pato la taifa kumedaiwa kuibuka kwa wimbi la madalali ambao wanatajwa kusababisha wizi wa matunda hayo mkoani njombe.


Baadhi ya wakulima wa parachichi mkoani Njombe akiwemo Alfred Msemwa,William Ngole na Zubery Ngimbudzi katika kikao kupitia asasi ya kusaidia wakulima ya Nshida wamesema kumekuwepo na wizi wa matunda yao kutokana na baadhi ya makampuni kuwatumia madalali ambao hawana mashamba wanaolazimika kwenda kuiba matunda majira ya usiku.


“Utakuta kuna kampuni inampa vifaa vya kubeba parachichi mtu bila kuangalia anakwenda kuchuma je analo shamba halafu mwisho wa siku unaskia kuna mkulima ameibiwa matunda”alisema Alfred Msemwa


“Wizi haupo mjini tu hapa sasa hivi kilimo hiki kimeingiliwa na madalali kwa hiyo thamani ya parachichi imeshushwa kupitia madalali,madalali wanaleta wateja wanakuja kuchuma mpaka saa nane za usiku sasa mtu anakuja mashambani anachunguza mchana akiona hapaingiliki anakuja usiku na tochi saa sita au saa saba anachuma na kwenda kuuza”alisema William Ngole


Mkurugenzi wa asasi ya NSHIDA bwana Frank Msigwa anasema tayari wamepata malalamiko hayo na wanatarajia kuitisha mkutano mkubwa wa wakulima wa Parachichi,makampuni ya ununuzi pamoja na serikali ili kujadili namna ya kukomesha suala hilo.


“Hii imekuwa ni changamoto kubwa sana,lakini tumeenda kuwasiliana na ofisi za serikali tumekubaliana tuandae mkutano wa wakulima wote Njombe ili kuliweka sawa hili”Alisema Frank Msigwa


Pamoja na changamoto hiyo lakini mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa hayajakata tamaa ya kuwasaidia wakulima kupitia asasi ya NSHIDA ambapo mkurugenzi msaidizi wa NSHIDA Adrian Byarugaba amesema wafadhali hao mbali na kilimo cha parachichi wameahidi kuwasaidia katika kilimo cha maharage jamii ya mikunde pamoja na pilipili kwa kuwajengea uwezo na kuwapa mitaji.


Amesema miongoni mwa mashirika yaliyoendelea kujitokeza ili kuwasaidia wakulima ni pamoja na Tanzania organic Agriculture movement (TOAM)  ambayo ni taasisi ya kilimo hai Tanzania itakayosaidia wakulima wa parachichi Njombe  kuwapa mafunzo ili waenelee kuzalisha mazao bora lakini pia taasisi ya GIZ kutoka Ujerumani itakayotoa ufadhili kwa wakulima 60 na kutoa mafunzo ya kilimo hai.Vile vile amesema taasisi ya Sustainable Agriculture  Tanzania (SAT) chuo cha  kutoa mafunzo ya kilimo hai kilichopo Morogoro wameendelea kushirikiana ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo.


Asasi ya NSHIDA hadi sasa ina takribani wanachama 5000 ambao ni wakulima wa parachichi pamoja na mazao hai ambao wamekuwa wakiunganishwa na masoko ya kimataifa kwa ajili ya kuuza mazao yao.