Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuongeza kutengeneza chanjo ya virusi vya corona barani Ulaya.
Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel amesema viongozi hao wamekubaliana pia katika mkutano wao wa kilele kuimarisha utoaji wa chanjo hizo kwa nchi wanachama.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amewaambia waandishi habari kwamba kwa upande mmoja wanaheshimu usambazaji wa chanjo za virusi vya corona ulimwenguni, lakini pia wanataka kuwalinda watu wao kwa sababu hiyo ndiyo njia ya kupambana na janga hilo. Siku ya Jumatano Umoja wa Ulaya uliongeza udhibiti wa mauzo ya chanjo za COVID-19 nje ya umoja huo katika juhudi za kukabiliana na uhaba wa chanjo.
Nchi za Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani ziko nyuma katika utoaji wa chanjo kuliko nchi zilizoko nje ya umoja huo kama vile Uingereza, Marekani na Israel.


0 Comments