TANGAZA NASI

header ads

JAMII YAASWA KUISHI KWA UPENDO NA WATU WENYE VVU, WATU WENYE ULEMAVU WASHAURIWA KUPIMA AFYA ZAO

 



 Na Maiko Luoga Njombe


Watanzania wameaswa kuto wanyanyapaa Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kwakuwa nao wanahaki ya kuishi na kufanya shughuli zao kwa kushirikiana na Jamii inayowazunguka.


Wito huo ulitolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe, Ummy Nderiananga aliposhiriki ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge inayohusika na masuala ya UKIMWI na Dawa za kulevya iliyotembelea Mkoani Njombe machi 02 na 03/2021 kwa lengo la kuona hali ya maambukizi ya VVU na Kifua Kikuu (TB) na kuagiza Elimu zaidi itolewe kwa Jamii.


Mhe, Ummy aliwataka Wananchi Mkoani Njombe na kote Nchini kuhakikisha wanajitokeza kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya kwa lengo la kupima na kujua Afya zao, wale watakaokutwa na Virusi hivyo waanze kutumia dawa za kufubaza makali na walioanza kuzitumia waendelee kuzingatia maelekezo ya Wataalamu wa Afya. 


Aidha alisema Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa Mikoa Nchini ambayo asilimia za maambukizi ya Virusi vya UKIMWI zipo juu hivyo Kamati ya Kudumu ya Bunge inayohusika na masala ya UKIMWI imetoa maelekezo kwa Serikali kuhakikisha inaongeza jitihada za kutoa Elimu kwa Jamii ili takwimu hizo ziendelee kushuka.


“Serikali tukiongozwa na jemedari wetu Mhe Rais Dkt, John Pombe Magufuli tuko imara kwenye mapambano dhidi ya VVU, Ili kuendeleza Taifa imara ambalo litaendelea kuchangia katika uchumi na Maendeleo ya Taifa letu” Alisema Mhe, Ummy Nderiananga.


Katika hatua nyingine Mhe, Ummy Nderiananga aliwashauri Watu wenye ulemavu Nchini kuhakikisha wanaondoa hofu wajitokeze kwenye Vituo vya Afya ili kupima na kutambua hali za Afya zao huku akiwataka Watanzania kutowatenga kwakuwa kufanya hivyo ni kuwaongezea msongo wa mawazo na kujikuta wapweke kwenye Jamii.


Mhe, Amandus Chinguile Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Mkoani Lindi na Mhe, Neema Mwandabila Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Songwe Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayohusika na masuala ya UKIMWI na Dawa za kulevya walisema pamoja na hali ya Maambukizi ya VVU kuwa juu katika Mkoa wa Njombe Wajumbe wamepongeza jitihada za Serikali za kupambana na hali hiyo.


Taarifa iliyotolewa na Dkt, Robert Masele Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Njombe kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge inayohusika na masuala ya UKIMWI na Dawa za kulevya ilionesha hali ya maambukizi ya VVU katika Mkoa wa Njombe imeshuka kutoka asilimia 14.8 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 11.4 mwaka 2017.

Post a Comment

0 Comments