TANGAZA NASI

header ads

DKT. ZAINAB CHAULA AKAGUA UJENZI WA PROGRAMU RUNUNU YA NAPA

 


Na Prisca Ulomi, WMTH

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula amekutana wa wataalamu wa TEHAMA wanaotengeneza Programu Rununu ya Anwani za Makazi na Postikodi (National Addressing and Postcode Mobile Application – NAPA) mjini Morogoro ili kukagua ujenzi wa programu hiyo unaotekelezwa na wataalamu hao

Dkt. Chaula amesema kuwa malengo ya Wizara ya kutengeneza programu rununu ya NAPA ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mfumo wa TEHAMA wa utambuzi wa maeneo ya makazi ya watu na kukusanya taarifa ili kuwezesha utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii nchini

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekweleza amesema kuwa programu rununu ya NAPA itakuwa na faida mbali mbali ikiwemo kusajili na kuhuisha anwani za makazi; kumwezesha mtumiaji kutambua mwelekeo wa anwani kwa kutumia ramani; kutambua mitaa/vitongoji vyote vyenye anwani za makazi; kumwezesha mtumiaji kutambua mwelekeo wa anuani kwa kutumia ramani; kutambua anuani za makazi kwa kutumia namba za TIN za TRA na za NIDA; kutambua maeneo yote ya huduma za kijamii na kiuchumi kama vile benki, polisi, ofisi za Serikali; kumwezesha mtumiaji kutambua umbali wa anuani kwa kutumia ramani; kumwezesha mwananchi kupata msaada wa huduma za dharura kwa urahisi na uharaka; na kuwezesha posta kuwafikia wateja wa huduma za posta kiganjani

Akiwasilisha taarifa ya utengenezaji wa programu hiyo kwa Dkt. Chaula kwa niaba ya wataalamu wengine, Mhandisi Jampyon Mbugi wa Wizara hiyo amesema kuwa ili kufanikisha utengenezaji wa programu rununu ya NAPA wataalamu wa TEHAMA wamekusanya mahitaji ya programu hiyo; usanifu wa mfumo; uundaji wa mfumo; majaribio ya mfumo; majaribio ya kukubali kwa mfumo huo kabla ya kufanya uzinduzi wa mfumo huo ambapo kazi hiyo imeanza kufanyika tarehe 12 Januari mwaka huu na utakamilika tarehe 28 Februari mwaka huu ili uanze kutumika

Naye Mhandisi Richard Magubila wa Wizara hiyo amesema kuwa programu rununu ya NAPA itaunganishwa na mifumo mingine ya TEHAMA ya Serikali kama vile ya kodi, ukusanyaji wa mapato, afya, biashara mtandao, ardhi, vitambulisho vya taifa na mifumo mingine ili kuwezesha kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kuendana na mahitaji, mabadiliko na ukuaji wa TEHAMA nchini

Wataalamu wanaohusika kuandaa programu rununu ya NAPA ni wataalamu wa ndani ya nchi yetu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Wizara ya Fedha na Mipango; Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee, Watoto na Ustawi wa Jamii; Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi; Shirika la Posta Tanzania; Wakala wa Serikali Mtandao; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania; Chuo Kikuu cha Dodoma; Chuo Kikuu cha Ardhi;  na wataalamu wa TEHAMA wa taasisi za sekta binafsi

Post a Comment

0 Comments