Na Mohamed Saif, Tarime
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka wataalam Sekta ya Maji kote nchini kutumia utaalam wao ili wananchi wapate huduma ya uhakika na toshelevu ya majisafi na salama
Ametoa maelekezo hayo Januari 5, 2021 wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa maji wa Gamasara Wilayani Tarime Mkoani Mara na kuzungumza na wanufaika wa mradi huo ambao kwa nyakati tofauti walimueleza changamoto zilizopo kwenye mradi.
Miongoni mwa changamoto zilizoelezwa na wananchi hao ni pamoja na mradi kushindwa kutoa maji inavyopasa kwani kuna wakati mabomba hua hayatoi maji.
Mara baada ya kujionea hali halisi ya mradi na maelezo ya wananchi wa maeneo husika, Waziri Aweso alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Rais. Dkt. John Pombe Magufuli ni kuwafikishia huduma ya maji wananchi wake na kwamba hatokubali kuwa kikwazo cha kufikiwa kwa dhamira hiyo na hivyo aliwataka wataalm wote kwenye Sekta ya Maji kujitathmini.
Waziri Aweso aliielekeza Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara kuhakikisha maboresho yanafanyika ili mradi uweze kutoa maji kama inavyopasa kwa lengo la kuhudumia wananchi wengi zaidi.
Alisema kuwa wananchi wanachohitaji ni maji na aliwaelekeza wataalam katika Sekta ya Maji kujiepusha na porojo badala yake wahakikishe wanajikita na kudumu kwenye falsafa ya maji bombani.
“Wataalam wetu kwenye Sekta ya Maji acheni porojo, elekezeni taaluma zenu na ubunifu katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero ya maji,” alielekeza Waziri Aweso.
Aliongeza “unapokuwa mtaalam lazima utoe ushauri kulingana na utaalamu wako, tunapoanzisha mradi maana yake ni wananchi wapate huduma, wataalam tutumie taaluma zetu kusaidia wananchi wapate maji,” alielekeza Waziri Aweso
Aidha, Waziri Aweso alizielekeza Jumuia za Watumia Maji kote nchini kuhakikisha zinasimamia vizuri miradi ya maji kwenye jumuia zao ikiwa ni pamoja na kuongeza umakini kwenye makusanyo kwa lengo la kuwa na miradi endelevu.
“Miradi mliyokabidhiwa inapaswa kuwa endelevu, sasa ni jukumu lenu kuhakikisha hili linafikiwa, hakikisheni mnashirikiana, mnaitunza na mnisimamia vizuri,” alielekeza Waziri Aweso.
0 Comments