Samirah Yusuph
Meatu. Juhudi za ziada kati ya wadau wa elimu, jamii pamoja na viongozi wa serikali katika kuhakikisha wanafikia malengo ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani hapa zimezaa matunda baada ya ukamilishaji kufikia asilimia 90.Wilaya ya Meatu ikiwa na jumla ya wanafunzi 4,135 wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Januari 11,2021 inajumla ya vyumba vya madarasa 62 kati ya vyumba 92 vinavyohitajika upungufu ukiwa ni vyumba 39.
Huku madawati yaliyopo ni 2,650 kati ya madawati 4,600 yanayohitajika na upungufu ukiwa ni madawati 1,950.
Ukamilishaji huo umelenga kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika wilaya hiyo wanapata nafasi ya kuanza masomo kwa wakati.
Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu Fabian Manoza alisema kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari ni zoezi endelevu ambalo linatekelezwa kwa muda mrefu.
Isipokuwa kulikuwa na majengo hitajika ambayo yalikuwa bado hayajakamilika kutokana na sababu mbali mbali hivyo kilichofanyika ni kuhakikisha wanahamasisha wananchi katika kukamilisha ujenzi ili wanafunzi wa kidato cha kwanza waanze masomo kwa wakati.
"Tumekuwa na ziara ya uhamasishaji kwa kushirikiana ambayo ni kamati ya ulinzi na usalama pamoja na kamati ya siasa, tumetembelea shule zote ambazo zilikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa tukajionea wenyewe ukamilishaji wa vyumba hivyo," Alisema Manoza na kuongeza kuwa;
"Hadi sasa majengo yote yaliyokuwa yanahitajika yapo tayari na tuna uhakika wa watoto wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari wataanza masomo yao bila kikwazo chochote na ifikapo Januari 15 tunatarajia kutembelea shule hizo ili kujihakikishia kama watoto wote wameanza masomo".
Akielezea mafanikio hayo Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Meatu Anthony Philipo alisema kuwa ufanikishaji huo ni matokeo ya muamko wa wazazi na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha watoto wanapata elimu.
"Kilichofanya kufanikisha kwa wakati ni mwitikio wa wananchi katika kuchangia nguvu kazi katika hatua ya ukamilishaji pamoja na utakelezaji mzuri wa majukumu wa watendaji wa serikali". Alisema Philipo na kuongeza kuwa;
"Ujenzi wa vyumba vyote vya madarasa haukutumia wakandarasi umetumia mafundi wa kawaida hivyo gharama za ujenzi ni nafuu na majengo yapo katika ubora wa hali ya juu".
Huku baadhi ya wananchi wakieleza kuvutiwa kwao na utendaji wa mkurugenzi wa Wilaya hiyo jambo ambalo linafanya wamuunge mkono kwa kushiriki nguvu kazi pale wanapohitajika kufanya hivyo.
"Anaye kushika mkono na yeye mshike kama viongozi wetu wa serikali tunawaona wanatufikia na kutuelewesha kuhusu watoto wetu kupata elimu ni lazima tushiriki kwa maana tunaona mchango wa pesa pamoja na nguvu zetu katika shule hizi zinazojengwa," Alisema Saguda Mwihu mkazi wa Kata ya Itinje.
Hadi hatua hii Halmashauri ya wilaya imechangia kiasi cha tsh milioni 360 katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, huku mwenyekiti wa halmashauri hiyo akiahidi kutoa kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo kutoka halmashauri katika vijiji ambavyo vitaonyesha ushirikiano mzuri wa nguvu kazi katika kuboresha miundombinu ya shule.
0 Comments