Na Amiri Kilagalila,Njombe
Changamoto ya uhaba wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya wilayani Ludewa mkoani Njombe ikiwemo hospitali ya wilaya hiyo, imeibua malalamiko miongoni mwa wakazi wa wilaya hiyo na kusababisha baadhi yao kulalamikia fedha zao za michango ya CHF.
Katika mikutano ya hadhara ya mbunge wa jimbo la ludewa Wakili Joseph Kamonga,diwani wa kata ya Ludewa mjini Monica Mchiro amesema changamoto ya uhaba wa dawa imekuwa ikimpa wakati mgumu kutokana na wananchi wake kumhoji mara kwa mara kauli iliyoungwa mkono na mwenyekiti wa ccm wilaya hiyo mzee Horace Kolimba.
“Watu waliolipa bima,wasiolipa wote wanaambiwa waende wakanunue dawa,na mimi nilipoliona na viongozi wangu taarifa tulizozipata pale ni kuwa kuna vyanzo vitatu vvya fedha lakini ni karibu mwaka mmoja na nusu ruzuku na fedha za basket fund hazijatolewa ndio maana kuna uhaba wa dawa na vifaa tiba,wananchi wanalalamika sana”alisema Monica Mchiro
Kwa kuliona hilo mbunge Kamonga amelazimika kufanya ziara katika hospitali ya wilaya ya Ludewa ili kuona uhalisia wa malalamiko hayo ambapo uongozi wa hospitali hiyo chini ya mganga mkuu wa wilaya Dokta Stanley Mlay umekiri kuwapo kwa changamoto hiyo miezi kadhaa iliyopita tatizo lililosababishwa na ugonjwa wa Corona lakini kwa sasa limetatuliwa na wananchi wanaendelea kupatiwa huduma huku mfamasia wa wilaya hiyo Seuri Mollel akieleza namna wanavyopata changamoto wakati wa kuagiza dawa MSD.
“Kulikuwa na upungufu mkubwa wa dawa kipindi cha nyuma lakini tumejitahidi kutatua hilo kadri ya uwezo wetu dawa za msingi zipo lakini kwa zile zitakazoelekea kupungua tutanedndelea kujitahidi kuongeza makusanyoili kuzuia upungufu wa mara kwa mara”alisema Dokta Stanley Mlay
“Tumepokea dawa za Milioni 22 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati na hospitali ya wilaya imepokea dawa za milioni 18 mwezi wa 11 “alisema mfamasia wa wilaya hiyo Seuri Mollel
Baadhi ya wagonjwa waliokutwa wakipatiwa matibabu katika hospitali hiyo akiwemo Ever Ngoye,Claudia Kidantu na Elnest Kowi wanasema wamekuwa wakihudumiwa vizuri huku wakiomba huduma kuendelea kuboreshwa zaidi.
“Tangu nimefika nimepokelewa vizuri,nimepima x ray kwasababu nasumbuliwa na mguu na tunashukuru sana kwasababu tunapata dawa vizuri”alisema Ever Ngoye
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga baada ya kutembelea na kukagua hospitali hiyo amejiridhisha na uwepo wa dawa za kutosha huku akiwataka wananchi kuendelea kwenda kupata huduma.
“Kufuatilia kero za wananchi kwenye huduma za afya ni wajibu wangu,tunajitahidi kukusanya mapato lakini bado hele ni chache sana inabidi tushirikiane kukusanya mapato ili serikali iweze kutoa huduma,nimeona hapa kuna dawa za kutosha ,madaktari wapo na huduma zinaendelea vizuri niwasihi madaktari muwahudumie wananchi kwa uzalendo na upendo”alisema Kamonga
Serikali ilipandisha bajeti ya dawa kutoka bilioni 60 hadi bilioni 290 ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa katika maeneo yote nchini
0 Comments