TANGAZA NASI

header ads

”Sasa ni megawati 580 zingine kutoka Ruhudji na Rumakali” Waziri Kalemani



Na Amiri Kilagalila,Njombe


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwa Mkoani Njombe Januari 30, 2021 amesema kuwa, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa miradi miwili mikubwa ya kufua umeme wa jumla ya megawati 580 kwa njia ya maji ambayo ni, Mradi wa Ruhudji na Mradi wa Rumakali yote kwa pamoja ikiwa Mkoani Njombe. 


Alieleza kuwa, Mradi wa Ruhudji utazalisha megawati 358 na Mradi wa Ruamakali utazalisha megawati 222 ambapo maandalizi ya ujenzi wa miradi hiyo miwili mikubwa yameanza utekelezaji wake kwa wakati mmoja ikiwemo maandalizi ya Miundombinu wezeshi kwaajili ya ujenzi rasmi wa miradi hiyo. 



“Utekelezaji wa Miradi hii ulianza kwa hatua ya kufanya usanifu  wa Miradi tangu Desemba 2020 na unakaribia kukamilika. Sasa tunatarajia kuingia hatua ya pili ya kutangaza zabuni ili kuwapata wakandarasi kuanzia mwezi Machi ili ifikapo mwezi Julai wakandarasi wawe wamepatikana na tuwakabidhi rasmi eneo la ujenzi ili waweze kuendelea na ujenzi‘’ alisema Waziri Kalemani 


Waziri Kalemani aliongeza kuwa, Miradi yote miwili inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu na hivyo kuongeza megawati 580 katika Gridi ya Taifa ili kuongeza uwezo ambapo kwa sasa Grid ya Taifa ina uwezo megawati 1602 tu. 


“Kwa mahitaji ya sasa, Nchi nzima tuna uwezo wa kutumia mpaka Megawati 1400, lakini kadri tunavyoongeza umeme katika Gridi, ndivyo tunavyo hamasisha na kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi toka nje na ndani ya Nchi, hivyo Serikali imeamua kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi hii miwili  ya Ruhudji na Ruamakali” alisema Waziri Kalemani.


Kwa upande wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Uzalishaji Umeme, Mhandisi   Pakaya Mtamakaya alisema sambamba na Miradi hiyo ya kufua umeme zitajengwa njia mbili za kusafirisha umeme huo za Msongo wa Kilovolti 400. 


“Njia ya kwanza itajengwa kutoka Ruamakali hadi Kituo cha Mwakibete Mbeya na ya pili kutoka eneo la Ruhudji mpaka kilipo kituo cha kupoza umeme Mkoani Iringa ili kuwezesha usafirishaji wa umeme huo kuingia katika Gridi ya Taifa na kutumika katika Mikoa mbalimbali nchini” alisema Mhandisi Pakaya.

Post a Comment

0 Comments