Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa wito kwa maafisa kilimo wa halmashauri za mkoa wa Morogoro kuwafundisha wakulima kanuni bora za kilimo cha umwagiliaji ili waongeze tija na uhakika wa kipato kufuatia serikali kuboresha miundombinu.
Ametoa wito huo leo wilayani Mvomero wakati alipokagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa ghala na skimu yaumwagiliaji ya kijiji cha Kagugu inayotekelezwa na Mradi wa kuongeza thamani zao la mpunga (ERPP).
” Wakulima lazima waoneshe kilimo bora kwa kutumia mbegu kidogo na maji kidogo kufuatia mafunzo waliyopatiwa na wataalam wa kilimo cha umwagiliaji ili tija ipatikanae na kuwasaidia kuongeza kipato kupitia zao la mpunga” alisema Kusaya.
Katibu Mkuu huyo ameagua mashamba ya mpunga kijiji cha Kagugu na kuwaelekeza maafisa kilimo wa halmashauri kuwafundisha wakulima kilimo cha kisasa ili mradi wa umwagiliaji uwasaidie kuongeza tija kwa kutumia eneo dogo kisasa.
Kusaya anafanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa mradi wa ERPP unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu Januari ili ukabidhiwe kwa wakulima kupitia halmashauri baada ya Wizara yake kukamilisha miradi yote kumi na moja.
Katibu Mkuu huyo wa Kilimo aliongeza kusema Mradi wa Kuongeza tija na uzalishaji wa zao la Mpunga (ERPP) unaotekelezwa kwa ubia na Benki ya Dunia umefanikiwa kujenga maghala (5),skimu za umwagiliaji (5) na ujenzi wa maabara moja ya kilimo kwa lengo la kusaidia wakulima kuongeza tija katika zao la mpunga hatimaye nchi ijitosheleze kwa chakula na kipato kwa wakulima.
“Lengo la Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ni kuona miradi hii ya kilimo cha umwagiliaji inamnufaisha mkulima,hivyo tutapenda kuona mara baada ya kuikabidhi kwa wakulima inakuwa endelevu” alisisitriza Kusaya.
Kusaya aliongeza kusema wizara yake inaamini kuwa kilimo cha umwagiliaji ndio mkombozi kwa mkulima kwani atakuwa na uhakika wa kuzalisha mazao yake zaidi ya mara moja katika mwaka kutokana na uwepo wa mabonde yenye maji na miundombinu ya kisasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinius Mugonya alisema wanaishukuru wwizara ya kilimo kwa kufanikisha kukamilisha miradi mitatu ya ujenzi wa maghala mawili kijiji cha Mbogo Kwamtonga na Kagugu pamoja na skimu ya umwagiliaji ya Kagugu ambazo zitakuza kiapato cha wakulima.
” Sisi wana Mvomero tuna miradi hii mitatu ambapo wakulima 5,673 watanufaika kwenye vijiji vya Mbogo Kwamtonga na Kagugu kwani tayari tija imefikia wakulima wanazalisha tani 5 hadi sita za mpunga kwa hekta” alisema Mugonya .
Mkuu huyo wa wilaya alisema mkakati wa wilaya yake ni kuhamasisha ujenzi wa viwanda vikubwa na vidogo ili kuongeza thamani ya zao la mpunga na kuwafanya wakulima wauze mchele badala ya mpunga ili wapate kiapato kikubwa.
Naye mratibu wa mradi wa ERPP Mhandisi January Kayumbe alisema kwa sasa miradiyote 11 katika wilaya za Mvomero, Kilosa na Ifakara ipo kwenye hatua za ukamilishaji na kuwa ifikapo mwisho wa mwezi huu itakakuwa tayari kukabidhiwa kwa wakulima.
Mradi wa ERPP ulianza kutekelezwa mwaka mwaka 2015 kwa gharama ya Dola za kimarekani milioni 22.91 toka Benki ya Dunia ukijusisha Tanzania Bara na Zanzibar.
Jumla ya miradi 11 ikiwemo ujenzi wa skimu 5 za umwagiliaji,ujenzi wa maghala 5 na ujenzi wa maabara moja ya mbegu inatekelezwa katika mkoa wa Morogoro chini ya ERPP.
0 Comments