Na Amiri Kilagalila,Njombe
Wakati matunda pori na mizizi yakitumika kama chakula katika zama za mawe za kale,kwa zama za sasa za chuma yameonekana kuwa matunda bora na ya kibiashara yanayowaingizia watu kipato cha kila siku.
Utajiri wa matunda pori mkoani Njombe unawapa fursa wenyeji wa mkoa huo kuyatumia kuboresha lishe pamoja na kibiashara.
Hata hivyo Mkoa wa Njombe umebarikiwa kuwa na matunda ya aina mbalimbali yakupandwa pamoja na matunda pori ambayo hustawi katika maeneo mengi ya porini.
Matunda yamekuwa yakiwapa fursa ya kibiashara wenyeji kama ilivyo kwa Theresia Mwajombe ambaye kila unapofika msimu wa matunda pori huchangamkia fursa kwa kwenda porini na kukusanya matunda kwa ajili ya biashara.
Kwa sasa ni msimu wa matunda pori wenyewe wanayaita masaulwa pamoja na makusu.
"Nikiokota huku porini naenda nyumbani nachukua mkeka,nayaanika harafu asubuhi nayaweka kwenye kapu harafu nayafunga na kuyapeleka mjini"alisema Theresia Mwajombe
Anachokifanya Theresia baada ya kukusanya matunda porini akiwa na kijana wake James Emilio ni kuyafungasha na kuyahifadhi vizuri na kisha kuyaagiza mjini kupitia vyombo vya usafirishaji ambako huwasiliana na wafanyabiashara wenzake ambao wanapokea na kuwajumlishia wafanyabiashara wengine Ikiwa kwa siku moja huokota zaidi ya debe tano na kila debe moja huuza kwa shillingi elfu mbili.
"Tukishayaokota huku porini tunayapeleka nyumbani na kuyahifadhi kwenye kihifadhio kizuri ili yafike mjini bila kupasuka pasuka"
Sabrina kapinga ni miongoni mwa wanaopokea matunda kutoka vijijini , akishayapokea huwauzia wanaojumua kwa ajili ya kwenda kuuza kwa rejareja kwenye vipimo vidogo.
"Kuna mtu anayenitaftia kule kijijini harafu namwambia apime debe na kwa mimi nachukua kuanzia debe tano na wateja ni wengi na akina wafanyabiashara ni wengi pia wanajishughulisha sana"alisema Sabrina kapinga
Wafanyabiashara hawa wanasema hawapati fedha nyingi lakini inayopatikana inawasaidia kujikimu Kimaisha Huku Walaji na watumiaji akiwemo Steward Mngalilwa wanaeleza namna wanavyofurahia kula matunda pori.
"Kuna watu wengine wanayaokota kule mdandu yanayodondoka chini na wanayaagiza kwenye gari,sahizi ndio msimu wenyewe,haya matunda hayana chemical yanasaidia kinga mwilini ndio maana wanyama wa porini wanaishi kwa ajili ya kula matunda haya"alisema Steward Mngalilwa
Pamoja na matunda pori wapo pia wanaojihusisha na shughuli nyingine za porini ikiwemo utegaji wa mizinga ya nyuki kwa ajili ya kujipatia asali.
0 Comments