Wadau mabali mbali mkoani Njombe na wageni kutoka mikoa jirani na Tanzania kwa ujumla,wanaendelea kunufaika na maonesho ya wiki ya chakula duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani katika halmashauri ya mji wa Njombe.
Rita Mbembati ni mkazi wa kambarage mjini Njombe na Mathias Chengula ni mkazi wa kijiji cha Iwawa kutoka wilayani Makete.Wanasema licha ya kujifunza mambo mengi juu ya chakula na lishe katika maonyesho lakini jambo la pekee ni namna walivyomtembelea mfugaji wa Ng'ombe wa maziwa kisasa na namna alivyofanikiwa katika lishe ili kuepukana na tatizo la udumavu kwa watoto.
"Ili tuepukane na hili tatizo la udumavu kwa watoto inawezekana hapa udumavu haupo ukiangalia hali aliyonayo huyu mkulima,na kwa Njombe tunafuga sana Ng'ombe na mkulima mwenzetu ametueleza anatumia karibu lita tatu kwa ajili yake mwenyewe"alisema Mathias Chengula
Rita Mbembati alisema "Mimi nilichojifunza kikubwa ni kumbe ujasiriamali upo na huyu mfugaji amenitia moyo aliposema alianza na Ng'ombe watatu na mimi hili nimelichukua,na tukiendelea kujifunza vitu kama hivi vizuri naona Njombe yetu itaepukana na hili tatizo la udumavu"
Joseph Kimwaia ni mfugaji wa Ng'ombe eneo la Lunyamwi mjini Njombe aliyetembelewa na wageni waliofika katika maonesho hayo.amesema awali alianza na ndama wa miezi mitatu lakini sasa amefanikiwa kuwa na Ng'ombe 15 wanaomuwezesha kupata lishe na kipato katika familia yake.
"Ng'ombe hawa wameniwezesha kupata lishe na kipato kwenye familia,wameniwezesha kujenga nyumba bora na hata usafiri wa pikipiki lakini bado wameniwezesha kutoa ajila kwa jamii inayonizunguka katika mashamba yangu"alisema Joseph Kimwaia
Enelina Mhigo ni mfugaji na mke wa mzee Kimwaia anasema ni vema jamii hususani wanawake wakashirikiana na waume zao katika ufugaji ili kupata mafanikio kwa kuwa mpaka sasa familia yake imeendelea vizuri kiuchumi.
Naye mkuu wa Idara ya mifugo halmashauri ya mji wa Njombe amesema moja ya majukumu ya msigi ya idara hiyo ni kusimamia huduma ya ughani na wanaendelea kushirikiana na mfugaji huyo katika majukumu mbali mbali yanayohusu mifugo yake.
"Huyu mfugaji wetu hapa moja ya vitu ambavyo tunazingatia ni kuhakiksha tunatoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa chambavu lakini pia mifugo hawa wanaogeshwa kila wiki pamoja na kuzingatia swala la matibabu na lishe kwa mifugo hao"alisema mkuu wa idara
Veronika Kesy ni mkuu wa wilaya ya Makete na mgeni wa heshima aliyeongozana na wageni kwa mkulima huyo mara baada ya kutoka sehemu ya maonesho kwa ajili ya kwenda kujifunza kwa wajasiliamali wa kawaida.Amesema licha ya kujifunza mengi na kutambua kuwa mfugaji huyo ni mfugaji bora, ni vema serikali ikanona namna ya kumuwezesha mkopo kwa ajili ya kupata kifaa bora cha kukamulia maziwa pamoja na ujenzi wa eneo la kuogesha mifugo.
"Tumeshauri wataalamu kuwa mfugaji huyu anaweza akasaidiwa mkopo akanunua mashine ya kukamulia maziwa ili kukamua kwa ubra bila kupoteza maziwa"alisema Veronika Kesy
0 Comments