Na Omary Mngindo, Chalinze

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze, wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Ridhiwani Kikwete, anawashukuru wakazi jimboni humo kwa kuonesha imani yao kwake.

Ridhiwani aliyepita bila kupingwa, akitetea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili akianzia mwaka 2015, ikitanguliwa kwa mwaka mmoja nyuma 2014 alipochaguliwa kwenye uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi iliyoachwa na mbunge Said Bwanamdogo aliyetangulia mbele za haki.

Alisema kuwa tangu kuanza kwa mchakato Kampeni jimboni humo ilipoanza amekuwa akipata usbirikiano mkubwa kutoka kwa wana-Chalinze, hatua onayothinitishwa kuungwa mkono na wananchi hao katika kuwaongoza katika kipondi kingine.

"Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunijaali afya njema pamoja na familia yangu, pili kwa kuniwezesha kupita pasipokupingwa, pia kutembea Kata zote 15 kufanya mikutano mizuri ya kampeni," alisema Ridhiwani.

Aliongeza kwa kuwashukuru wakazi hao kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano hiyo, na kuwasikiliza yeye na msafara mzima ukiongozwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya hiyo, huku akisema kwamba hatowaangusha.

"Dhamira yangu ni kuendelea kuwatumikia kama ilivyokuwa kipindi kinachoishia 2020, nitaendelea tena kwa kipindi cha mpaka 2025 ili kuhakikisha kwa pamoja tunashirikiana kutekeleza shughuli za kimaendeleo, pia kutatua changamoto, tumedhamiria kuiona Chalinze kuwa jimbo lenye ukarimu, upendo na maendeleo," alisema Ridhiwani.

Aidha amewaomba wana-Chalinze kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi Octoba 28 kumpatia kura za kishindo mgombea Urais Dkt John Magufuli na Wagombea Udiwani wa CCM katika kata 6 kati ya 15, ambazo ni Kibindu, Mbwewe, Miono, Mkange, Ubena na Bwilingu.

"Katika siku chache zilizobaki kabla ya siku ya kupiga kura nitaendelea kupita na kufanya mikutano kwenye baadhi ya kata, ili kuwahimiza wana Chalinze wenzangu kujitokeza kwa wingi kupiga kura," alimalizia Ridhiwani.

Aidha alimshukuru Dkt. Magufuli kwa kazi kubwa aliyowafanyia wana-Chalinze kwa kuanzia na Hospitali ya Wilaya iliyopo Msoga, mradi mkubwa wa maji unaotokea chanzo cha mto Ruvu, ujenzi wa daraja kubwa mto Wami na miradi mbalimbali jimboni humo.