Rais Kyrgyzstan Sooronbai Jeenbekov ametangaza kujiuzulu leo katika juhudi za kumaliza msukosuko ambao umelikumba taifa hilo la Asia ya Kati baada ya uchaguzi wa bunge uliopingwa.
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake, Jeenbekov, ambaye amekabiliwa na miito ya ajiuzulu kutoka kwa waandamanaji na wapinzani wa kisiasa, amesema kubakia madarakani sio jambo la maana kwa umoja wa nchi na makubaliano ya kijamii.
Amesema kwake yeye, umoja wa nchi, umoja wa watu na utulivu wa jamii ni muhimu zaidi kuliko mambo mengine yoyote.
Tangazo hilo limekuja siku moja tu baada ya Jeenbekov kupuuza sharti la kumtaka ajiuzulu kutoka kwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, akisema atabakia madarakani hadi pale hali ya kisiasa katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 6.5 itakapotulia.
0 Comments