KOCHA mpya wa Yanga Mrundi, Cedric Kaze, amewatumia ujumbe mkubwa mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kwa pamoja watafanya makubwa.
Kauli hiyo aliitoa kocha huyo akiwa njiani kutua hapa nchini akitokea Canada ambapo makazi yake yalikuwa huko.
Kocha huyo anakuja kuifundisha timu hiyo baada ya kufikia makubaliano mazuri na mabosi wa Yanga akichukua nafasi ya Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyetimuliwa Oktoba 3.
Kaze amesema:-“Ninajivunia kuwa kocha mpya wa Yanga, timu yenye historia nzuri ambayo mashabiki wake ni wazuri.
“Yanga ni kati ya timu bora katika ukanda wa Afrika, kwa pamoja tutafanya makubwa, kikubwa kinachotakiwa ni ushirikiano na kupeana sapoti katika majukumu ambayo nitayaanza.
"Ninatambua kwamba kuna ushindani mkubwa ukizingatia kila timu imejipanga kufanya vizuri ili ipate matokeo chanya, ninaamini kila kitu kitakuwa sawa," amesema.
Kaze atatua saa nne usiku na moja kwa moja atajiunga na kambi ya Yanga iliyowekwa kwenye Kijiji cha Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam tayari kwa ajili ya kuanza kibarua cha kukinoa kikosi hicho.
0 Comments