TANGAZA NASI

header ads

TTCL wasaini makubaliano na ZICTIA

 


NA THABIT MADAI, ZANZIBAR.

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imetiliana saini makubaliano ya kuunganisha mkongo wa mawasiliano wa taifa na Wakala wa Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar(ZICTIA).

Akizungumza katika hafla ya utiliaji saini huo iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Kisauni Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mwasiliano sekta ya mawasiliano Dk. Zainab Chaula amesema hatua hiyo kuunganishwa kwa mkongo huo wa mawasiliano wa Taifa utaleta fursa pekee kwa watoa huduma wa mitandao visiwani Zanzibar kuweza kuyafikia masoko ya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Dk.Zainab amesema, mkongo wa mawasiliano wa taifa wa Zanzibar na Tanzania Bara umeunganishwa kupitia njia mbili ya Tanga hadi Pemba,Dar es Salaam mpaka Unguja na kwamba mkongo huo utatoa fursa kwa visiwa vyote vya Unguja na Pemba kupata mawasiliano ya uhakika na kwa wakati wote.

Amesema mkongo wa huo wa mawasiliano wa taifa umetengenezwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya sh.bilion 630 na wenye urefu wa umbali wa kilomita 7,910 na umefika kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Amesema ni wazi kuwa uwepo wa mkongo wa Zanzibar ambao umeunganishwa kwenye mkongo huo wa mawasiliano wa taifa unatarajia kufungua fursa kwa wawekezaji na watoa huduma mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe amesema, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) imetumia zaidi ya sh.bilion 30 kuunganisha mitambo hiyo katika mikoa yote ya visiwani vya Unguja na Pemba na wilaya zake. 

Pia,Katibu Mkuu huyo amewataka Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Kindamba na Mtendaji Mkuu wa ZICTIA,Mhandisi Shukuru Suleiman kuhakikisha kuwa, miundombinu ya mawasiliano ya mkongo huo inasimamiwa kikamilifu kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ili wananchi waendelee kunufaika na huduma za mawasiliano.

Akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa upande wa TTCL, Mkurugenzi mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba alisema, tukio hilo linafanyika baada ya kukamilika kwa hatua zote muhimu za kitaalamu na kiufundi kwa pande zote mbili.

Mkurugenzi huyo alisema, ufunguzi wa njia ya mawasiliano ya mkongo huo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa na manufaa makubwa sana kwa Taifa ikiwemo kuwezesha kuongezeka kwa matumizi ya huduma za data na intarneti.

Alisema lakini pia kuongeza uwekezaji wa kampuni za mawasiliano kwa upande wa Zanzibar na hivyo kukuza mapato ya Serikali hizo mbili.

Post a Comment

0 Comments