Mkuu wa kanisa la KKKT,ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mkoani Kilimanjaro Askofu Dkt.Fredrick Onael Shoo amewataka viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuwahamasisha waumini wao kuombea uchaguzi mkuu pamoja na kuchagua viongozi wenye uadilifu wenye kuchukia vitendo vya rushwa.
Akiongoza ibada ya kumstaafisha msaidizi wa Askofu mchungaji Paulo Elipokea Urio,Dkt.Shoo amesema kuwa katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu oktoba 28 mwaka huu ni vyema watu wakachagua viongozi waadilifu wenye hofu ya Mungu na wanaochukia rushwa kwani rushwa ni adui wa haki ambapo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kampeni kusikiliza sera ili kuweza kufanya maamuzi sahihi siku ya uchaguzi.
"Nitumie fursa hii kuwasihi wa wakristo na watanzania kwa ujimla ili muweze kuchagua kiongozi wenye sifa ambao watakuwa wa kwanza kupiga vita vitendo vya rushwa kwa kujitokeza kwenye kampeni zinazofanywa na vyama mbalimbali kusikiliza sera zao pia nanyi wakristo kwa nafasi yenu napaswa mkatae rushwa kwa namna yeyote ile na msikubali kutumiwa na watu kwa manufaa yo."alisema Dkt.Shoo
Aidha Dkt.Shoo amewataka wakristo kuendelea kumtegemea Mungu na siyo kutumia akili zao wenyewe huku wakifahamu kuwa ndani ya kristo ni familia moja hivyo amewataka kuzidi kuitenda kazi ya Bwana siku zote maana katika utendaji kazi huo ndimo kuna thawabu yake Kristo.
Vilevile amewataka viongozi na waumini wote kuona umuhimu wa kujua msingi wa imani yao na kuisimamia katika kuwaongoza watu kwani wakristo wengi hawana ufahamu wa kutosha katika kile wanachokiamini ndiyo maana imani zao zinatikishwa kila wakati.
Akifungua Mkutano Mkuu wa 14 wa Dayosisi ya Meru uliofanyila Chuo Kikuu cha Makumira Askofu wa Dayosisi ya Meru Mch.Elias Kitoi ameeataka wajumbe wa mkutano huo kudumisha umoja walionao kwa mafanikio ya dayosisi na jimbo kwa ujumla ambapo pia amemtaka kila mloja kujaribu kutenda haki ya urai kwa kujiandikisha na kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.
"Tushirikini mkutano huu mkuu kwa kutoa mawazo chanya ya kwenda mbele na ni imani mkutano huu utawaimarisha,utawatuliza na utakuwa mkutano wa kiroho ili mkazidi sana kuitenda kazi ya Bwana siku zote mkijua ya kwamba taabu yenu si bure katika Bwana maana yeye atawafikisha salama."Alisisitiza Askofu Kitoi
Akitoa salamu za serikali ya mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddy Kimanta,Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro katika mkutano huo ametoa taarifa ya mwenendo wa uchaguzi mkuu mpaka kufikia Septemba 20 mwaka huu katika wilaya yake kuwa mpaka kufikia nuru ya mchakato huo hakuna fujo wala vurugu zilizotokea kutokana na maombi ya wakristo ambapo amewaomba wajumbe wa mkutano huo kuendelea kuiombea nchi hususani katika uchaguzi mkuu kwani taifa linahitaji maombi ili kuweza kuvuka salama katika uchaguzi huo ambao kila mtanzania anayo haki na fursa ya kupiga kura na kuchagua kiongozi anayefaa.
Ameongeza kuwa serikali ya wilaya inaungana na kanisa hilo katika kushukuru kwa magumu yote ambayo nchi imeyapitia ikiwemo janga la Covid 19 ambapo kwa maombi ya wakristo na kufunga kwao na kuendelea kumlilia Mungu ndiko kulikosababisha nchi kuvuka salama katika janga hilo na kuongeza kuwa kwa muda wa miaka miwili wameona utulivu wa kanisa na kushuhudia kuona likiungana na serikali katika kutoa huduma za kiroho na kimwili kwa waumini na wananchi kwani imekuwa ni miaka miwili ya mafanikio makubwa kwa kazi ambazo kanisa limefanya iliwemo ufanyaji wa harambee za ujenzi wa makanisa mbalimbali pamoja na kuimarisha kasi na kiwango cha utoaji wa huduma za kiroho kwa wananchi.
Ameeleza kuwa yapo mambo mbalimbali ambayo serikali ya awamu ya tano imeyafanya na kupelekea nchi kuingia katika historia duniani kwa kutambuliwa na kuonekana kuingia kwenye uchumi wa kipato cha kati kwani yapo mataifa mengi yalitamani kuwa mataifa ya uchumi wa kati lakini nchi ya Tanzania Mungu ameipendelea na ataendelea kuwa pamoja nayo
Naye Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati Dkt.Solomon Masangwa amesema kuwa mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili ni mafanikio ambayo yanakuja tena kwa miaka inayofuata hivyo amewataka wajumbe wa mkutano huo wasimuoache Bwana ambapo pia amegusia suala la uchaguzi mkuu ambapo amewakata wajumbe hao kujitokeza kupiga kura na kuchagua kiongozi bora atakayewatumikia kwa maendeleo ya wananchi.
Awali akisoma historia ya utumishi wa mstaafu huyo,Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Meru amesema kuwa Mchungaji Paulo Elipokea Urio alizaliwa mwaka 1955 katika kijiji cha Sing'isi Wilayani Arumeru na kubatizwa mwaka 1965 na kuanza kutumika katika kazi ya Bwana mnamo mwaka 1977 kama mchungaji ambapo mwaka 1981 alibarikiwa kuwa mchungaji katika Usharila wa Poli na mwaka 2002 hadi mwaka 2018 alitumika kama msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Meru.
Sambamba na hayo Msaidizi huyo Mstaafu amewashukuru wakristo wote wa Dayosisi Meru kwa kumuenzi kutokana na kazi alizotumika takribani miaka 39 ambapo amewaomba wana dayosisi kwa ujumla kudumisha mshikamano na upendo miongoni mwao huku kila mmoja akijituma katika kumtumikia Mungu.
0 Comments