Na James Timber, Mwanza.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Misungwi Mkoani Mwanza imefanikiwa kuokoa fedha jumla ya Milioni 18.27 ikiwemo kiasi cha Milioni 10 zilizokuwa zimechukuliwa na mkopeshaji kwenye akaunti ya Mwalimu Mstaafu, Augustine Ngowi (62) kwa njia isiyo halali.
Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Takukuru Mkoa Emmanuel Stenga, Mkuu wa Takukuru wa Wilaya hiyo Emma Mwasyoge alisema mwalimu huyo baada ya kustaafu na kulipwa mafao yake zaidi ya milioni 95 baadaye jumla ya sh. 14,900,000 zilikuchukuliwa kwenye akaunti yake na mkopeshaji kwa njia isiyo halali.
Mwasyoge alisema uchunguzi umebaini mhusika wa tukio hilo ni mkopeshaji anayefahamika kwa jina la Emmanuel Chacha (32) ambaye alimukopesha mwalimu kiasi cha Sh. 3,490,00 kuanzia novemba 2018 hadi april 2019 ambapo walikubaliana kulipana mkopo huo kwa riba ya 20% kwa kila mwezi.
Alisema Mwalimu Ngowi baada ya kuingiziwa fedha zake za mafao kwenye akaunti yake, Emmanuel Chacha alikwenda benki na kubaini uwepo wa fedha hizo na baadaye kufanikiwa kuhamisha kiasi cha sh. 14,900,000 kutoka kwenye akaunti ya mwalimu huyo kwa kuwa alikuwa anashikiria kadi ya benki na namba ya siri ya akaunti ya mwalimu huyona takukuru baada ya kujiridhisha walimuhoji mtuhumiwa ambaye alikiri kosa na kukubali kurejesha kiasi cha sh. 10,000,000.
Katika hatua nyingine Emma Mwasyoge alisema Takukuru wilayani humo imefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh. 1,227,000 zilizokuwa zimetumiwa vibaya na viongozi wa kata na vijiji katika mradi wa ukamilishwaji wa maboma ya Shule ya Sekondari Igokelo ambapo baada ya uchunguzi viongozi wa kijiji cha Busolwa na wale wa kata walibainika kuhusika ambapo walikiri kosa na kurejesha pesa hizo.
Alibainisha, ofisi hiyo imeokoa upotevu wa sh. 7,050,000 fedha za makusanyo ya mapato kwa kutumia mashine za kielekroniki ambazo hazikuwasilishwa na wahusika kwenye akaunti ya kukusanyia mapato ya ndani na wahusika walikiri kosa na tayari wamesharejesha pesa hizo takukuru na Kufanya Jumla ya pesa zote zilizookolewa mwezi june na Takukuru Misungwi kuwa Sh. 18,277,000 ambapo aliwataka wakopeshaji wote kufuata sheria pasipo kukandamiza mtu.
Mwalimu Mstaafu Augustine Ngowi aliishukuru Takukuru kwa kumusaidia kurejesha pesa hizo ambapo aliwashauri watanzania wote ikiwemo walimu kuwa makini na mikopo inayotolewa mitaani kwani mingi inaambatana na riba pamoja na mashariti kandamizi ambayo yanaweza kuwafilisi na kushindwa kufaidi matunda ya kazi zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Samwel Sweda aliipongeza Takukuru kwa kuokoa fedha za wanyonge kitu ambacho kinadhihirisha utendaji kazi wao unaunga mkono kauli ya Rais Magufuli ambaye mara kadhaa amekuwa akisisitiza serikali yake kuwa ni ya wanyonge.
0 Comments