TANGAZA NASI

header ads

RC Ole Sendeka amuapisha DC mpya wa Wanging’ombe mkoani Njombe




Na Amiri Kilagalila,Njombe

Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher  Ole Sendeka amemuapisha mkuu mpya wa wilaya ya Wanging'ombe Bw,Lauteri John Kanoni na kumtaka kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kikatiba na utawala bora bila kujali hadhi ama cheo cha mtu.

Akizungumza wakati akimuapisha mkuu huyo wa wilaya ambaye ameteuliwa kuchukua nafasi ya Comrade Ally Kassinge akitokea mkoani Songwe alikokuwa akihudumu katika nafasi ya katibu tawala msaidizi idara ya serikali za mitaa Olesendeka amemtaka mkuu huyo wa wilaya kuchapa kazi kwa bidii huku akizingatia kuwa mwajiri wake namba moja ni mwananchi na kutoa onyo kwa viongozi wanaotumia nafasi yao vibaya.

“Kasumba ya hivi karibuni ninayoiona ambayo inakinzana na sera za msingi za Chama chetu,misingi ya utu,na kuna mengine yanatia kichefu chefu wewe mkuu wa wilaya mkuu wa mkoa unafika kwenye mkutano wa hadhara wananchi wanasubiri utelemke wakupokee,hushuki kwenye gari mpaka atoke e mtu wa kukufungulia mlango sasa najiuliza mkono wako wa kushoto umelemaa au tatizo lake ni nini”alisema Sendeka

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa amempongeza aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Ally Kasinge kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa katika kipindi chote cha uongozi na kumuagiza mteule mpya kwenda kufanya ziara kijiji kwa kijiji haraka iwezekanavyo ili kujua maeneo yote ya wilaya kabla uchaguzi mkuu haujafanyika.

“Tunatarajia pia mkuu wa wilaya ufanye ziara haraka sana ya kuielewa Wanging’ombe,kuelewa kwanza kata uliyonayo na vijiji ulivyo navyo lakini pia kujua siasa za ndani zinazoendelea”alisema Ole Sendeka

Wakati  akila kiapo Lauteri Kanoni ameahidi kupitia kiapo hicho kuto muangusha Rais wa Jamhuri ya Muungano na serikali

“Naahidi kupitia kiapo hiki sitamuangusha Mhe,Rais pamoja na wewe mkuu wa mkoa na viongozi wote wa mkoa wa Songwe ili tuweze kutekeleza majuku tunayopewa mara kwa mara na viongozi wetu”alisema Lauteri Kanoni

Mtangulizi wake Comrade Ally Kassinge wakati akiaga hapo jana baada ya kuweka bayana nia yake ya kugombe ubunge katika jimbo la Kilwa Kusini alisema anaondoka akiwa amefanikiwa kuinua sekta ya elimu,afya,miundombinu pamoja na mshikamano baina ya watumishi na wananchi.

Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli Julai 07,2020 alifanya uteuzi wa Mkuu huyo wa wilaya mmoja na wakurugenzi wa Halmashauri watano katika mikoa mbalimbali. 
Rais Magufuli alimteua Lauteri Kanoni kuwa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe akichukua nafasi ya Ally Kasinge,ambapo kabla ya uteuzi huo Kanoni alikuwa Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Serikali za Mitaa huko Mkoani Songwe.




Post a Comment

0 Comments